Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Makala

Mizani ya uhuru wa uchumi haupimi kwa kiwango cha misaada pekee

PROFESA Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), amesema kuwa Tanzania imepunguza kwa kiwango kikubwa utegemezi wa misaada ya nje, hivyo kusitishwa au kuwekwa masharti kwenye misaada hakutakuwa na athari kubwa kama ilivyokuwa zamani.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 15:15Dakika 3 kusomaToleo 177, uk. 33 & 34

Anasema masharti ya misaada hayana tena athari ya kimkakati katika uamuzi wa serikali, kwani tayari imejumuisha hatari ya kupungua au kusitishwa kwa misaada hiyo katika mfumo wake wa usimamizi wa fedha za umma.

Pia alieleza kuwa utegemezi wa misaada katika bajeti ya serikali umeshuka kwa kiwango kikubwa katika miaka ya karibuni, kwamba serikali imeendelea na sera ya kuongeza mapato ya ndani na kujitegemea katika kugharamia maendeleo, hivyo nafasi ya misaada kwenye bajeti imeendelea kupungua.

Kauli ya Prof. Kitila Mkumbo inaweza kuchambuliwa kwa jicho la sera za uchumi wa kimataifa bila kuikataa au kuikubali moja kwa moja.

Hoja kuu siyo misaada imepungua, bali kama Tanzania imejenga kiwango cha juu cha uhimilivu wa uchumi, kinachoweza kuhimili misukosuko ya nje bila athari kubwa.

Kwa mtazamo wa uchumi wa kimataifa, utegemezi wa misaada ni kipimo kimoja tu cha uhuru wa kiuchumi.

Hivi sasa nchi nyingi hazidhibitiwi tena kupitia misaada pekee; ushawishi umehamia katika masoko ya fedha, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI), mikopo ya mashirika ya fedha ya kimataifa, teknolojia, minyororo ya thamani duniani, mifumo ya malipo ya kimataifa, na upatikanaji wa masoko ya kimataifa.

Hivyo, hata kama misaada inapungua, hilo pekee halimaanishi kuwa uwezo wa nje wa kuathiri uchumi wa taifa umepungua kwa kiwango hicho hicho.

Aidha, historia ya uchumi wa dunia inaonyesha kuwa vikwazo vya kisasa havijikiti tena katika kusimamisha misaada. Mara nyingi hulenga upatikanaji wa mitaji, uwekezaji, huduma za kifedha, uhamishaji wa teknolojia, au imani ya wawekezaji.

Katika mazingira hayo, kauli kwamba “vikwazo vya misaada haviwezi kufanya kazi tena”

inaweza kuwa sahihi katika muktadha mwembamba wa misaada, lakini siyo lazima iwe sahihi katika maana pana ya shinikizo la kiuchumi la kimataifa.

Pia, uhuru wa kiuchumi haupimwi kwa kiwango cha misaada pekee, bali kwa uwezo wa taifa kugharamia matumizi yake kupitia mapato ya ndani, kuwa na msingi mpana wa kodi, sekta binafsi yenye ushindani, uzalishaji wenye thamani ya juu, na uwezo wa kuuza bidhaa na huduma zenye ushindani katika soko la dunia.

Bila misingi hiyo, kupungua kwa misaada kunaweza kuwa matokeo ya mabadiliko ya sera za wafadhili badala ya ushahidi wa kujitegemea kikamilifu.

Kwa upande mwingine, ikiwa serikali imejumuisha hatari ya kupungua kwa misaada katika mfumo wa usimamizi wa fedha za umma, hiyo ni hatua ya usimamizi wa hatari.

Lakini usimamizi wa hatari hauondoi hatari yenyewe; unasaidia kujiandaa nayo. Hivyo kauli hiyo haipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa uchumi sasa hauwezi kuathiriwa na shinikizo za nje.

Katika muktadha wa kimataifa, nchi zinazotajwa kuwa na uhuru mkubwa wa kiuchumi, kama vile Korea Kusini, Singapore, au Norway hazikufikia hatua hiyo kwa sababu ziliondoa utegemezi wa misaada pekee, bali kujenga taasisi imara, kuongeza tija ya uzalishaji, kuwekeza katika elimu na teknolojia, kuboresha utawala wa sheria, na kuifanya sekta binafsi kuwa injini ya ukuaji wa uchumi.

Hivyo, kipimo cha kweli cha kujitegemea ni uwezo wa uchumi kuendelea kukua, kuvutia uwekezaji, na kustahimili mishtuko ya dunia bila kutegemea hatua za dharura.

Kwa hiyo, swali la msingi siyo kama misaada imepungua, bali – Je, Tanzania imejenga uchumi unaoweza kustahimili mabadiliko ya masoko ya dunia, kupungua kwa uwekezaji wa nje, mabadiliko ya bei za bidhaa, na misukosuko ya kifedha ya kimataifa bila kuyumba?

Hicho ndicho kipimo kinachotumiwa na wachumi wengi duniani kutathmini kiwango halisi cha mamlaka ya kiuchumi.

Kwa mtazamo huo, kauli ya Prof. Kitila inaweza kueleweka kama ujumbe wa kisiasa na kiutawala kuhusu maendeleo ya usimamizi wa fedha za umma.

Hata hivyo, kutoka katika uchambuzi wa uchumi wa kimataifa, ni hitimisho pana linalohitaji kuungwa mkono na viashiria vinavyoonyesha uwezo wa uchumi wa taifa kujitegemea katika uzalishaji, mapato ya ndani, ushindani wa kimataifa, na ustahimilivu dhidi ya shinikizo mbalimbali kutoka nje.

Mwandishi ni mtafiti, mchambuzi na msomaji mkubwa wa Pambazuko.

  • Uchumi
  • Misaada
  • Kitila Mkumbo

Soma Pia