Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Msomi ataka takwimu kukua uchumi ziguse jamii

MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Sanaa Bunifu, Dkt. Dominicus Makukula, amesema wakati umefika kwa wataalamu kueleza sababu za kukua kwa uchumi wa nchi, wakati Watanzania wengi bado wako kwenye lindi la umasikini.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 06:00Dakika 3 kusomaToleo 182, uk. 15

Amehoji kuwa wakati takwimu zinazotolewa kila wakati na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zikionyesha kuwa uchumi wa Tanzania unakua, iweje watu wake waendelee kuwa masikini.

Akizungumza na Pambazuko katika mahojiano maalum, Dkt. Makukula, amesema utafiti unaofanywa kuhusu ukuaji wa uchumi wa Tanzania unapaswa kueleza sababu na njia za kukomesha umasikini unaoonekana wazi.

Dkt. Makukula ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Utumishi wa Kitaalum la UDSM (Udasa), ameshauri pia kuwa ukuaji wa uchumi katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma kusichukuliwe kuwa kielelezo cha uchumi wa nchi nzima kukua.

Msomi huyo amesema kuna aina fulani ya shughuli zinazofanyika katika maeneo hayo na hivyo kuyafanya kuwa kielelezo, kunashindwa kuonyesha ukweli kuhusu hali ya umasikini ambao umekithiri mikoa mingi ya pembezoni.

Dkt. Makukula amesema miaka michache iliyopita takwimu hizo zilionyesha kuwa Tanznaia imeingia kwenye uchumi wa kati wa juu, lakini baadaye ikarekebishwa kuonyesha kuwa ni uchumi wa kati wa chini, jambo ambalo limezidi kuwachanganya wananchi.

“Tunapaswa kuwa tunaona huo utafiti. Matokeo ya utafiti yawafikie watu waweze kuona thamani ya kuwajibika kwao na kupima namna wanavhochangia ukuaji wa uchumi wao,” amesema.

Anabainisha kuwa ukifuatilia hali ya Dar es Salaam utabaini kuwa baadhi ya watu wana uchumi mzuri sana na wakati huohuo, wapo wenye uchumi mbaya zaidi. “Wakati wewe unahangaika kutafuta shilingi hamsini, kuna jamaa jirani yako anaporomosha ghorofa la vyumba 30 hadi, mpaka unachoka, wengine wanabadilisha magari, lakini wewe huna hata baiskeli,” anasema.

Mhadhiri huyo anasema mambo hayo ni lazima yaangaliwe na kuzingatiwa katika utafiti ili majibu yashabihi hali halisi ya maisha ambayo Watanzania wengi wanaishi. “Hivyo vitu lazima viangaliwe, ninamini kukua kwa uchumi wa nchi ni sawasawa na baba katika familia yake. Kama zamani kipato chake kilikuwa Shilingi 150,000, uchumi ukikua anapaswa kupata chakula kizuri mwezi mzima...”

“Baba ambaye mtoto wake walikuwa anatembea bila viatu, sasa aweze kumudu kununua jozi tatu au nne za viatu. Kama mke alikuwa anavaa malapulapu, aanze kuvaa nguo nzuri, hiyo ndiyo tafsiri ya kukua kwa uchumi,” anasema msomi huyo.

Soko la ajira nchini Dkt. Makukula amezungumzia ubora wa elimu katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla, ambapo amesema taasisi za elimu zinapaswa kuwa na mitaala ambayo inaendana na matakwa ya soko la ajira.

Amesema UDSM kila wanapotaka kuandaa mitaala mipya, lazima washirikishe wadau katika sekta husika, akieleza kuwa Shule Kuu ya Biashara ambao wamekuwa wakishirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya mabenki kwenda kutoa ushauri wa wataalam wanaowahitaji. Katika mahojiano hayo, Katibu huyo wa Udasa amesifu mabadiliko makubwa katika kuandaa mitaala ya elimu ya vyuo vikuu yaliyofanywa na serikali ya China hivi karibuni.

Amesema serikali ya nchi hiyo imefuta program za shahada ya kwanza zaidi ya 1,200 na kuleta kozi ambazo zinaendana na masuala ya ubunifu katika sayansi kwa kuangalia nafasi yao, mahitaji na ushindani walionao duniani.

“Wachina kuna baadhi ya mambo mazito wameyaondoa kwenye shahada na sijui wameyapeleka wapi.

Kwa mfano degree (shahada) ya sanaa wameiondoa, na nyingine zinazohusiana na masuala ya sayansi ya jamii, nyingi wamezifuta. Wenzetu Wachina wameangalia mahitaji na mabadiliko ya kielimu na ushindani wa kidunia” amesema Dkt. Makukula.

  • Uchumi
  • Takwimu
  • Jamii

Soma Pia