Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Michezo

Mtanzania aweka historia soka la wanawake Marekani

Hakika Tanzania inaendelea kuchanja mbuga katika michezo, tayari binti wa Kitanzania ameweka historia ya kutukuka huko Marekani. Fuatilia hapa kujua kilichompa sifa hiyo.

Jumatatu, 5 Oktoba 2026 · 19:15Dakika 2 kusoma
Clara Luvanda akiwa ametinga jezi ya timu yake mpya, Washington Spirit.
Clara Luvanda akiwa ametinga jezi ya timu yake mpya, Washington Spirit. — Picha kutoka mtandaoni

MWANADADA kutoka Tanzania, Clara Luvanga, ameandika historia baada ya kufunga bao la ushindi na kuisaidia Washington Spirit kuichapa Houston Dash mabao 3-2, katika mchezo wa ligi ya wanawake nchini humo.

Bao hilo, lililopatikana dakika ya 84, lilivunja sare ya mabao 2-2 na kuifanya Washington iondoke na pointi tatu katika Uwanja wa Shell Energy, Houston, Texas, Jumapili - Oktoba 4, 2026.

Luvanga amekuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kufunga katika Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake Marekani, maarufu kama NWSL.

Dakika sita kabla ya kumalizika kwa muda wa kawaida, mshambuliaji huyo alipokea pasi ya Claudia Martínez iliyomweka katika nafasi ya kukabiliana na kipa, Jane Campbell. Hakupoteza nafasi hiyo, akafunga bao lililoamua mchezo na kuipa timu yake sababu ya kushangilia.

Washington ilikuwa imeongoza mara mbili, lakini kila ilipoonekana kupata mwanya wa kuelekea kwenye ushindi, Houston ilirudi mchezoni na kusawazisha.

Tara Rudd alianza kuifungia Washington dakika ya 11 kwa kichwa, baada ya kona iliyopigwa na Esme Morgan.

Miljana Ivanović aliwasawazishia wenyeji kabla ya mapumziko, baada ya kutumia kosa la kuondosha mpira katika eneo la hatari. Timu hizo zilienda mapumzikoni zikiwa zimefungana bao moja kila klabu.

Kipindi cha pili, Sofia Cantore aliirudisha Washington mbele dakika ya 51, akimalizia pasi ya Trinity Rodman katika shambulizi la kushtukiza. Hata hivyo, Ivanović alifunga tena dakika ya 59 na kurejesha sare.

Hapo ndipo Luvanga, aliyeingia kipindi cha pili, alipogeuka tofauti kati ya timu hizo. Bao lake liliokoa Washington kuondoka na sare baada ya jitihada zake za kutafuta ushindi kukwamishwa mara mbili.

Huu ulikuwa mchezo wake wa pili tangu kujiunga na klabu hiyo, hatua inayolifanya bao lake kuwa mwanzo wenye matumaini katika mazingira ya ushindani.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, TFF, lilithibitisha kwamba Luvanga alijiunga na Washington Spirit akitoka Al Nassr ya Saudi Arabia, kwa mkataba unaomfikisha mwishoni mwa msimu wa 2029.

Aliondoka Saudi Arabia akiwa na historia ya mafanikio, ikiwemo mataji matatu mfululizo ya ligi na kiatu cha dhahabu baada ya kufunga mabao 24 msimu uliopita.

Kwa soka la wanawake Tanzania, bao hili lina maana inayovuka ushindi wa Washington kwani linatoa mfano kwa wasichana kwamba safari ya kutoka nyumbani hadi kushindana kimataifa inawezekana, huku likimpa Luvanga msingi wa kuendelea kujithibitisha katika ligi hiyo na kuanza kuwa kipenzi cha wapenda soka wa Marekani na dunia.

  • clara luvanda
  • soka
  • marekani
  • bao

Soma Pia