Habari
Mwalimu Nyerere alifanya nini zaidi ya wengine?
Mchakato wa kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa Mtakatifu unaendelea. Hatua hii inaleta maswali mengi kuhusu mwanasiasa, tena kutoka nchi masikini, akifika huko, je alifanya nini chenye utukufu zaidi ya wengine? Soma hapa kujua zaidi.

MTU aliyewahi kuongoza nchi, kusimamia jeshi na kusimamia rasilimali za mabilioni ya fedha, sasa yuko katika mchakato wa kuelekea kutangazwa kuwa Mtakatifu wa Kanisa Katoliki.
Jina lake ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Rais Tanganyika na baadaye Tanzania, baada ya nchi hiyo kuungana na Zanzibar mwaka 1964.
Lakini mwanasiasa aliwezaje kufikia hatua ya kutarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu? Ni mambo gani aliyoyafanya tofauti?
Wakati baadhi ya marais wa Afrika walipokuwa wakitajirisha familia na kujijengea himaya za mali, Mwalimu Nyerere alikuwa akijenga misingi ya aina nyingine.
Oktoba 11, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Lazarus Msimbe, aliwaambia maelfu ya waumini waliokusanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrick kwamba; “Endeleeni kumuombea Mwalimu. Miaka 27 baada ya kifo chake, safari yake kuelekea utakatifu imeanza.”
Tangu mwaka 2005, Vatican imemtambua rasmi Mwalimu Nyerere kama mtumishi wa Mungu (Servant of God), hatua ya kwanza katika mchakato wa kumtangaza mtu kuwa Mtakatifu katika Kanisa Katoliki.
Kwa mujibu wa ujumbe huo, mchakato wake sasa umefikia hatua ya kuwahoji mashahidi. Hatua zinazofuata ni kutangazwa kuwa mwenye heshima (Venerable), kisha mwenye heri (Blessed), na hatimaye Mtakatifu (Saint).
Uongozi bila kujitajirisha kwa wizi
Katika kipindi ambacho baadhi ya viongozi wa Afrika walikuwa wakitajirika kwa kushika madaraka, Mwalimu Nyerere alifariki bila kujulikana kuwa na akaunti za fedha nje ya nchi, majumba ya kifahari nje ya nchi au himaya kubwa za biashara.
Baada ya kustaafu, alirejea kijijini kwake Butiama mkoani Mara na kujishughulisha na kilimo.
Uadilifu ulikuwa utajiri wake
Mwalimu Nyerere aliongoza taifa lake kwa ushawishi, si kwa vitisho. Askofu Msimbe alinukuliwa akisema; “Alikuwa mwalimu, si dikteta.”
Mwalimu Nyerere hakuhitaji kutumia askari kuwalazimisha watu wamsikilize, silaha yake kubwa ilikuwa uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha, kutoa hoja zenye mantiki na kuwaheshimu wengine.
Aliweza kukosoa bila kumdhalilisha mtu, aliongoza bila kutumia nguvu kuwalazimisha watu kukubaliana naye, huo ni mfano wa uongozi unaotajwa kuwa adimu katika siasa za Afrika.
Aliishi kwa kuzingatia kanuni
Falsafa yake ya ujamaa haikuwa sera ya kisiasa pekee, bali pia ilihusishwa na mtindo wake wa Maisha, alithamini unyenyekevu, upendo kwa watu maskini na maisha yasiyojaa anasa.
Alijulikana kwa kuvaa mavazi rahisi, yakiwamo suti za mtindo wa Kaunda, wakati viongozi wengine wa Afrika walipendelea mavazi ya gharama kubwa kutoka kwa wabunifu wa kimataifa.
Mwalimu Nyerere aliamini kuwa uongozi ni huduma kwa watu, si njia ya kujipatia hadhi na kujitukuza.
Alikabidhi madaraka kwa hiari
Mwaka 1985, Nyerere aliamua kwa hiari kuachia madaraka ya urais, wakati ambapo viongozi wengi Afrika walikuwa wakishikilia madaraka kwa muda mrefu.
Uamuzi wake ulikuwa ishara ya msimamo wake kwamba viongozi hawapaswi kung'ang'ania Madaraka kwa muda wote.
Hatua hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa mifano muhimu ya uongozi wa kuwajibika katika historia ya Afrika.
Funzo kwa viongozi wa leo
Wakati waumini wakiendelea kumuombea Mwalimu Nyerere katika safari yake ya kutangazwa kuwa Mtakatifu, yapo maswali muhimu yanayoibuliwa na ujumbe wa Askofu Msimbe; Ikiwa Nyerere aliweza kuwa mnyenyekevu akiwa Ikulu, kwa nini viongozi wetu wa leo washindwe kuwa wanyenyekevu wanapokuwa madarakani?
Ikiwa Nyerere aliweza kuwa mwadilifu akiwa na mamlaka ya kusimamia rasilimali nyingi za taifa, kwa nini wengine washindwe kuwa waaminifu hata wanaposimamia bajeti ndogo?
Ikiwa rais anaweza kuishi kwa uadilifu kiasi cha kuanzisha safari ya kuelekea kutangazwa kuwa Mtakatifu, kwa nini diwani ashindwe kuishi kwa misingi ya uaminifu na maadili?
Mwalimu Nyerere hakuiongoza Tanzania pekee. Alionyesha Afrika kuwa inawezekana kutumia madaraka kama dhamana ya kulitumikia taifa, badala ya kujinufaisha binafsi.
Na ndiyo maana, kwa mujibu wa ujumbe huu, Kanisa Katoliki linaona kuwa maisha yake yanastahili kuchunguzwa katika mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu.
Makala haya yameandikwa na mwandishi kutoka Nigeria.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Mwalimu Nyerere
- Utakatifu
- Tanzania
- Uongozi