Habari
Mwisho wa enzi! Ronaldo atangaza kustaafu rasmi Ureno
Mwanasoka galasa wa Ureno, ametangaza kuacha kuichezea timu ya taifa lake, akieleza kwamba anastaafu ili kupisha damu changa zaidi.

MECHI 234, mabao 146 na miaka 23 ya historia, hatimaye Cristiano Ronaldo anafunga ukurasa wa safari yake ya kuitumikia Timu ya Taifa ya Ureno baada ya kuweka rekodi za kipekee katika soka la dunia.
Ronaldo, ambaye amekuwa alama ya mafanikio na fahari kwa soka la Ureno, ameandika historia isiyosahaulika kupitia rekodi zake za mabao, uongozi na mataji mbalimbali aliyoyapata akiwa na timu hiyo.
Katika ujumbe wake wa kuaga, Ronaldo amesema; watu wa Ureno, umefika wakati wa kuirudisha jezi namba 7 ya timu yetu ya taifa. Wakati umefika wa kuikabidhi kwa vizazi vijavyo."
Katika kipindi chake cha kuitumikia Ureno, Ronaldo ameshiriki katika mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwemo Kombe la Dunia na michuano ya EURO. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, amefunga mabao 146 katika michezo 234, huku akisaidia timu hiyo kutwaa mataji muhimu.
Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni ubingwa wa EURO 2016 pamoja na mataji mawili ya UEFA Nations League mwaka 2019 na 2025.
Hata hivyo, safari yake imekuwa na changamoto mbalimbali. Kumekuwa pia na taarifa za mvutano wake na benchi la ufundi kufuatia kutoridhishwa na uamuzi wa kiufundi kuhusu nafasi yake katika kikosi.
Ureno haitakuwa inaaga tu mchezaji, bali itakuwa inaaga kizazi cha kipekee kilichobadilisha historia ya soka lake.
Ronaldo anaondoka akiwaacha mashabiki na kumbukumbu za mabao, rekodi, mataji na nyakati ambazo zitabaki katika historia ya mchezo wa soka.
Unamkumbuka Cristiano Ronaldo kwa lipi zaidi? Je, ni mabao yake ya kihistoria, ubingwa wa EURO 2016, uongozi wake ndani ya uwanja au uwezo wake wa kuamua matokeo katika nyakati muhimu?
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Ronaldo
- Mpira
- Ureno
- Kusaafu