Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Tanzania yalipa mabilioni ‘kujisogeza’ kwa Trump

Tanzania pamoja na nchi zingine za Afrika, imebainika kuingia mikataba na kampuni za ushawishi ili kuifikia Ikulu ya Marekani kwa lengo la "mazungumzo rasmi."

Alhamisi, 17 Septemba 2026 · 11:51Dakika 7 kusomaToleo 182, uk. 6
Jengo la Ikulu ya Marekani- almaarufu White House
Jengo la Ikulu ya Marekani- almaarufu White House — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

SERIKALI kadhaa za Afrika, Tanzania ikiwemo, zinalipa mamilioni ya dola kwa kampuni za ushawishi nchini Marekani zenye uhusiano na mtandao wa kisiasa na kikazi wa Rais Donald Trump.

Lengo la malipo hayo ni kupata fursa kubwa zaidi ya kufikia na kujisogeza zaidi kwa Marekani; nchi tajiri zaidi kwa fedha, uchumi imara na nguvu kubwa za kijeshi.

Idara ya Haki ya Marekani – kupitia Sheria ya Usajili wa Mawakala wa Kigeni (FARA), inaitaja Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika kwamba uhusiano wao na Marekani umetetereka baada ya kukumbwa na mwenendo wa kisiasa “ulioshindwa kuifurahisha Marekani.”

Pambazuko limebaini kuwa nchi hizo, pamoja na Tanzania ni Kenya, Nigeria, Rwanda, Morocco, Somalia na Angola, ambazo sasa zinalipa mabilioni ya shilingi “kuhuisha zaidi uhusiano na Marekani.”

Serikali za nchi hizo zinaelezwa kulipa kuanzia mamia ya maelfu hadi mamilioni ya dola, ili kupata “sikio la Ikulu ya Rais Donald Trump na Serikali ya Marekani.

Tanzania yajitosa zaidi Gazeti la Pambazuko limeona sehemu ya maelezo ya taarifa inayotokana na mkataba ulioingiwa na Tanzania - kupitia FARA, kuwa Tanzania imesaini mkataba na kampuni ya BGR Government Affairs wenye thamani ya dola za Marekani milioni tatu kupitia usajili namba 5430, uliotiwa saini Juni 18, 2026. Mkataba huo utadumu kwa miezi 12.

Malipo hayo ya dola za Marekani 250,000 (zaidi ya Shilingi milioni 650) kwa mwezi, yataigharimu Tanzania karibu Shilingi bilioni 8 kwa mwaka.

Hata hivyo, pamoja na kulipa mabilioni hayo kwa “kujiweka karibu na Ikulu ya Marekani,”

Tanzania – kupitia mkataba huo, itafanya kazi karibu na kampuni moja ya ushawishi ya Hispania, Drift Advisors, ambayo imethibitika kuwa na “uzoefu kwa kazi za namna hiyo. Kufikia Ikulu ya White House ya Marekani.”

Kumbukumbu za FARA zinataja kampuni hiyo ya Hispania kama mpatanishi anayefanya kazi kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa pia mkataba mwingine wa Ervin Graves Strategy Group, ambao unaripotiwa kuwa na thamani ya dola za Marekani 45,000 (zaidi ya Shilingi milioni 117) kwa mwezi, hivyo kuifanya Tanzania kutumia takribani dola milioni nne (zaidi ya Shilingi bilioni 10.4) katika ushawishi nchini Marekani.

Mtaalamu wa Uchumi wa Diplomasia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Walter Nguma, anasema matumizi ya kampuni hizo kwa ajili ya kufanya ushawishi kwa serikali za mataifa makubwa ni njia ambayo imekuwa ikitumika kwa miaka mingi hasa pale inapotokea kwamba nchi haina namna ya kujisaidia kuwafikia wahusika moja kwa moja.

Hata hivyo, Dkt. Nguma anaonya kuwa njia hii siyo nzuri kwa sababu ni kiashiria cha kuzorota kwa wenye majukumu ya kuimarisha diplomasia baina ya nchi.

Anasema nchi inapoanza kutumia kampuni hizo siyo ishara nzuri kwa sababu katika hali ya kawaida nchi inatakiwa kutumia balozi zake katika nchi husika ambazo zina maofisa ambao wanalipwa mishahara na kutengewa kasma kwa ajili hiyo.

“Hii siyo ishara nzuri kwa diplomasia ya kisiasa na kiuchumi kwa kuwa inaonyesha kutowajibika ipasavyo na ni namna ya matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma kwa sababu lazima uainishe kwamba unatumia kampuni hizo ili kusaidia nini, nchi inanufaika vipi kwa hatua hiyo...”

“Hii inaingiza nchi katika kutumia utaratibu usiokuwa sahihi wa matumizi ya fedha za umma suala ambalo ni hatari katika uwajibikaji...”

“Ila inaweza kuwa jambo zuri kwa upande mwingine hasa nchi inapoona kwamba haiwezi kufikia malengo katika eneo hilo kwa kutumia jitihada zake binafsi na inaonekana kuwa Tanzania imelazimika kuingia katika utaratibu huo hasa kutokana na mbinyo unaotokana na yale yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025,” anasema.

Alisema kampuni hizo zipo katika nchi nyingi zikiwemo Uingereza, mataifa mengine ya Ulaya na hata Urusi, ambapo hutumia ukaribu Deus Kibamba na ushawishi wao kuzikutanisha serikali za nchi mbalimbali na serikali ya nchi tajiri pale uhusiano wa kidiplomasia unaposhindwa kutekeleza jukumu hilo.

Anaeleza kuwa inapotokea hivyo, hiyo ni fursa kubwa kwa kampuni hizo kuvuna fedha nyingi kwa muda mfupi kulingana na matukio, lakini inashauriwa kwamba isiwe utamaduni kwa serikali zinazotajwa kuona kwamba ndio mtindo wa uendeshaji wa mambo yao.

Kibamba achambua Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Deus Kibamba, amesema hatua hiyo haina afya kwa taifa na inaondoa morali ya wataalamu wengi walioajiriwa katika Wizara ya Mambo ya Nje.

“Wapo wataalamu lukuki katika eneo hilo waliohitimu kikamilifu na wengine wakiwa wanaendelea kufundisha katika vyuo vikuu vya ndani, wangeweza kutumika kwenye suala hilo,”

anasema Kibamba katika mahojiano na Pambazuko.

Kibamba anasema baadhi ya nchi huzitumia kampuni hizo mara chache hasa kama ina upungufu wa wataalamu katika eneo fulani, hasa kwenye taaluma adhimu, lakini hali haiko hivyo kwa Tanzania ambayo imeshajenga uwezo wa kutosha kwa wataalamu wake.

“Hii inaweza kueleweka kama wanahitajika wataalamu wa eneo mahsusi na baada ya kujichunguza mkabaini kuwa hamna wataalamu wa aina hiyo, ndipo mnapotafuta wataalamu kutoka nje...”

“Jambo hili linalofanyika sasa - ukiangalia msingi wake ni kutokana na yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana,” anaongeza.

Anasema hata kama wataalamu wa ndani hawana ufanisi wa kutosha, serikali ilitakiwa kuwakodi hao wanaoona kwamba wana weledi na ufanisi zaidi ili waje “kuwanoa” wataalamu wa ndani kwenye maeneo yenye upungufu.

Msomi asema anena Dkt. Ismail Kamweri wa Taasisi ya Kupunguza Umasikini (TPRI) anasema Tanzania inafanya vyema kutumia kila mwanya kujiweka jirani na wale alioita “wakubwa.”

Amesema kutokana na “kuchafuka kwa sifa ya amani ya Tanzania,” ni sahihi kwa nchi kuwematokeo mazuri.

“Hizi ni juhudi za kutaka kuficha jambo, lakini siku zote ukweli haufikiwi wala haufichwi, maana kama lingekuwa suala la kidiplomasia wanadiplomasia wangefanya kazi yao, lakini kwa kuwa hili ni zaidi, ndiyo sababu kuna mahangaiko ya kukodi kampuni za nje kutaka kuzitumia kujisafisha,” amesema.

Amesema juhudi hizo ni kupoteza fedha za umma pasipo sababu ya msingi kwa kuwa hata Serikali ya Marekani haiwezi kukubali kufichwa kwa uovu kwa kutumia kampuni hizo za ushawishi.

Kenya nayo yajisogeza Pambazuko pia limeona Kenya katika jalada la FARA lenye namba ya usajili 7545, Agosti 6, 2025 kwamba ilisaini mkataba wa ushawishi wa dola za Marekani 175,000 (zaidi ya shilingi 455 milioni) kwa mwezi kwa kipindi cha miezi 12 (hivyo kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 5.4) kabla ya mazungumzo ya Rais William Ruto na Rais Trump katika Ikulu ya White House.

Nigeria haijabaki nyuma Nigeria nayo pia ilisaini mkataba wenye thamani ya dola milioni tisa kwa mwaka na DCI Group, kampuni yenye uhusiano na baadhi ya watu wa ndani wa kampuni za Rais Trump.

DCI ni kampuni ya ushauri wa masuala ya umma inayotoa huduma kamili, inayobobea katika mawasiliano na huduma za ushauri wa kimkakati kwa zaidi ya miaka 25.

Rwanda nayo haijapoa Pambazuko limeona sehemu ya mkataba wa Rwanda na Kampuni ya Yorktown Solutions kama kampuni iliyosajiliwa kwa ajili ya kufanya shughuli za ushawishi, huku Rwanda Development Board (RDB) ikiwa ndiyo mhusika wa kigeni anayewakilishwa. Hii ilikuwa Machi 31, 2025 Rais Donald Trump ka - kwa washawishi huko Marekani.

Morocco hawana mchezo Taarifa zilizopo chumba cha habari cha Pambazuko zinaonyesha kuwa Morocco ilitumia kiasi cha dola milioni 3.49 (zaidi ya Shilingi bilioni 8.8) kwa shughuli za ushawishi nchini Marekani mwaka 2025, ikitafuta kuendelea kupata uungwaji mkono na Marekani kwa msimamo wake kuhusu Sahara Magharibi.

Somalia wajikongoja Somalia tayari imesaini makubaliano ya dola 600,000 (zaidi ya Shilingi bilioni 1.5) na BGR Group ili kufanya ushawishi na Marekani ili kuitambua Somaliland kama nchi huru.

Angola wanang’ang’ana Angola imethibitika kulipa dola 312,500 (zaidi ya Shilingi 812.5 milioni) kwa mwezi kwa kampuni yenye uhusiano na maofisa wa zamani wa Trump ili kuutambulisha zaidi Ushoroba wa Lobito, njia muhimu ya kusafirisha madini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Msumbiji haitaki mchezo Kampuni ya Brownstein Hyatt Farber Schreck iliingia mkataba na Msumbiji ili kuiwakilisha kwenye ushawishi kwa Marekani.

Iliingia mkataba na kampuni hiyo na kuilipa dola za Marekani 40,000 (zaidi ya Shilingi milioni 104) kwa mwezi kwa kipindi cha miezi 12, hivyo, thamani ya mkataba huo kwa mwaka kufikia dola 480,000 (zaidi ya shilingi bilioni 2.2).

Uganda nayo imo Julai 9, 2026, kampuni ya Skyline Capitol iliwasilisha marekebisho ya kimfumo kuongeza Ubalozi wa Jamhuri ya Uganda kuwa mhusika wa kigeni, ikiwa na jukumu la kuishauri Serikali ya Uganda kupitia ubalozi wake kuhusu mawasiliano na watunga sera nchini Marekani.

Gharama zake hazikuweza kutambulika haraka kwa Pambazuko.

  • ikulu
  • marekani
  • tanzania

Soma Pia

Tanzania yalipa mabilioni ‘kujisogeza’ kwa Trump | Pambazuko