Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Ndejembi aunguruma UN

Aiambia dunia kuwa madeni na mikopo ghali vinakwamisha nchi zinazoendelea kujenga miundombinu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Jumatano, 23 Septemba 2026 · 18:36Dakika 4 kusoma
Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi akihutubia Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa.
Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi akihutubia Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa.

Na Mwandishi Wetu, New York

Tanzania imezitaka nchi duniani kufanyiwa mageuzi makubwa kwenye mfumo wa fedha, ikisema gharama kubwa za mikopo, kuongezeka kwa mzigo wa madeni na ugumu wa kupata mikopo ya muda mrefu kwa masharti nafuu vinazinyima nchi zinazoendelea nafasi ya kuwekeza kwa kasi katika miradi ya maendeleo.

Hayo yamesemwea na Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, katika Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, Marekani, ambako anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Hoja ya Tanzania imekuwa ni sehemu ya mjadala mpana miongoni mwa nchi zinazoendelea zinazotaka mabadiliko katika mfumo wa kimataifa wa fedha, zikieleza kuwa gharama za kupata mitaji zinaathiri uwezo wao wa kugharamia miundombinu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutekeleza mipango mingine ya maendeleo ya muda mrefu.

“Wakati nchi zinazoendelea zinapoongeza kasi ya maendeleo, zinakabiliwa na gharama kubwa za mikopo, mzigo unaoongezeka wa madeni na upatikanaji mdogo wa fedha nafuu za muda mrefu,” Ndejembi aliuambia mkutano huo.

Ndejembi alihimiza kuongezwa kwa mikopo yenye masharti nafuu, mitaji ya sekta binafsi, kurahisisha upatikanaji wa fedha za maendeleo na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuongeza uwakilishi wa nchi zinazoendelea katika vyombo vinavyofanya uamuzi kuhusu mfumo wa fedha duniani.

Fedha ghali, maendeleo ghali

Hoja hiyo ina maana kubwa kwa nchi zinazoendelea kwa sababu gharama ya fedha haiishii katika bajeti na madeni ya serikali pekee.

Serikali inapokopa kwa gharama kubwa, uwezo wake wa kuwekeza katika umeme, barabara, reli, maji, afya, teknolojia na miradi inayohimili athari za mabadiliko ya tabianchi unaweza kubanwa.

Miundombinu hiyo ndiyo pia inayotegemewa na sekta binafsi katika uzalishaji na uwekezaji.

Kwa mtazamo huo, Tanzania inasema haiwezekani nchi zinazoendelea zikatarajiwa kuongeza uwekezaji ili kufikia malengo ya maendeleo ya kimataifa huku zikipata mitaji kwa masharti yanayopunguza uwezo wao wa kufanya uwekezaji huo.

Suala hilo linazidi kuwa muhimu wakati dunia ikielekea mwaka 2030, ukomo uliowekwa kwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Ndejembi alisema kasi ya dunia kufikia malengo hayo bado hairidhishi na akataka mkazo zaidi uwekwe katika utekelezaji na matokeo yanayopimika ya fedha zinazotumika katika maendeleo.

“Tanzania inaendelea kuwa na dhamira ya kutekeleza Ajenda ya 2030,” alisema.

Fedha za tabianchi nazo kitendawili

Ndejembi alizungumzia pia upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alibainisha kuwa nchi zinazoendelea zinakabiliwa na gharama zinazoongezeka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, wakati huohuo zikihitaji mabilioni ya fedha kuwekeza katika kujenga uwezo wa kukabiliana na athari hizo na kuhamia katika mifumo ya uchumi yenye uzalishaji mdogo wa hewa ukaa.

Makamu wa Rais ametaka kurahisishwa kwa upatikanaji wa fedha za tabianchi na maendeleo kutoka kwenye nchi zilizoendelea, sambamba na kuongeza mitaji binafsi.

Alisema kuwa kwa nchi kama Tanzania changamoto ni namna ya kutumia fedha chache za umma kuvutia mitaji mikubwa zaidi ya sekta binafsi katika miradi yenye tija ya miundombinu na maendeleo.

Ataka mageuzi Umoja wa Mataifa

Tanzania pia imetaka mageuzi hayo yasibaki katika mfumo wa fedha pekee, bali yafike ndani ya Umoja wa Mataifa wenyewe.

Ndejembi alisema UN inapaswa kubadilika ili kuendana na hali ya sasa ya dunia bila kudhoofisha jukumu lake la kusaidia maendeleo.

“Kusimamia mabadiliko kunahitaji kuufanyia mageuzi Umoja wa Mataifa ili uendane na hali halisi ya nyakati zetu,” alisema.

Alipongeza juhudi za Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, kupitia mpango wa UN80.

Tanzania yataka kiti Baraza la Usalama

Katika hatua nyingine yenye uzito wa kidiplomasia, Ndejembi ametangaza rasmi nia ya Tanzania kuwania kiti kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030.

Uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwaka 2028.

Kwa mujibu wa msimamo uliowasilishwa, Tanzania ikichaguliwa inakusudia kuongeza sauti ya Afrika katika masuala ya amani na usalama, kusisitiza diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani.

Azma hiyo ni sehemu ya hoja pana kwamba nchi za Afrika na mataifa mengine yanayoendelea yanahitaji uwakilishi mkubwa zaidi katika taasisi za kimataifa zinazofanya maamuzi yanayogusa fedha, maendeleo, amani na usalama.

Msimamo kuhusu Palestina

Ndejembi pia alizungumzia mgogoro wa Israel na Palestina, akieleza wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu Gaza na Mashariki ya Kati kwa ujumla.

Alitaka raia kulindwa, misaada ya kibinadamu kuruhusiwa kufika bila vikwazo na juhudi za kidiplomasia kuongezwa ili kupata suluhu ya kudumu.

Tanzania imerudia kuunga mkono suluhu ya mataifa mawili, Israel na Palestina, kuishi kwa amani na usalama kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, huku ikisisitiza haki ya Wapalestina ya kujiamulia mambo yao.

“Tumesimamia msimamo huu kwa miaka 50 iliyopita. Kwetu sisi, hili ni suala la misingi ya sera yetu ya mambo ya nje,” alisema Ndejembi.

Soma Pia