NSSF yarekodi mafanikio makubwa
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita NSSF imepata mafanikio makubwa katika maeneo ya miradi, makusanyo ya michangi, uandikishaji wanachama na uimara wa mfuko.

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kurekodi mafanikio ya kihistoria katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia mwaka 2025/26.
Hatua hiyo imesababishwa na maboresho ya mifumo ya TEHAMA, kuongezeka kwa wawekezaji, pamoja na mazingira wezeshi ya kibiashara yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, masha Mshomba, amesema.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mfuko huo mbele ya Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam, Mshomba amesema Mfuko umeshuhudia ukuaji mkubwa wa thamani yake, makusanyo ya michango, idadi ya wanachama, pamoja na kasi ya ulipaji wa mafao kwa wastaafu na wanufaika.
Thamani ya Mfuko na vitega uchumi
Mkurugenzi Mkuu huyo alibainisha kuwa thamani ya Mfuko wa NSSF imekua kwa asilimia 125, kutoka shilingi trilioni 5.06 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia shilingi trilioni 11.41 mwezi Juni 2026.
Wakati huo huo, Mshomba amesema thamani ya vitega uchumi vya Mfuko nayo iliongezeka kwa asilimia 108, ikipanda kutoka shilingi trilioni 4.62 mwaka 2020/21 hadi shilingi trilioni 9.60 mwaka 2025/26.
"Ukuaji huu mkubwa unathibitisha kuwa NSSF ipo imara na endelevu. Ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa thamani ya vitega uchumi, michango ya wanachama pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji katika miradi mbalimbali ya kimkakati," alisema Mshomba.
Wanachama na michango
Katika kipindi hiki husika, ambacho kilikuwa ni utekelezaji wa mpango mkakati wa saba wa NSSF, Mfuko uliandikisha wanachama wapya 1,486,930, hatua iliyofanya idadi ya wanachama wachangiaji kuongezeka kwa asilimia 130 kutoka wanachama 932,112 mwezi Juni 2021 hadi kufikia wanachama 2,144,906 mwezi Juni 2026.
Kufuatia kuongezeka kwa wanachama na kuimarika kwa uthibiti na mifumo ya ukaguzi, makusanyo ya michango kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 147, kutoka shilingi trilioni 1.17 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi trilioni 2.90 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2026.
Maboresho ya mafao
Katika kuwahudumia wastaafu, Mshomba amesema kuwa Mfuko umefanya maboresho makubwa kwenye viwango vya mafao. Alibainisha mathalani kuwa malipo ya mafao ya mkupuo yaliongezeka kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35, huku kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kikipanda kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000.
Aidha, amesema viwango vya pensheni kwa wastaafu wengine vimeongezeka kati ya asilimia 2 na asilimia 20.
Katika kipindi hicho, malipo ya mafao kwa wastaafu na wanufaika yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 594.33 (2020/21) hadi shilingi trilioni 1.16 mwaka 2025/26.
Mshomba alifafanua kuwa Mfuko umefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kushughulikia na kulipa madai.
Amesema wastani wa siku za kulipa madai yaliyokamilika umepungua kutoka siku 63 mwaka 2021 hadi kufikia siku 19 tu mwezi Juni 2026.
Aidha, asilimia 99 ya madai ya mafao yaliyofunguliwa yamelipwa ndani ya muda wa kisheria wa siku 60.
Skimu ya HIFADHI kwa waliojiajiri
Ili kufikisha huduma za hifadhi ya jamii kwa wananchi walio katika sekta isiyo rasmi, Mshomba amesema Mfuko ulizindua Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi waliojiajiri (Skimu ya HIFADHI) mwezi Februari 2026. Skimu hii inawalenga wakulima, wavuvi, waendesha bodaboda, machinga, mamalishe na wajasiariamali waliojiajiri katika sekta nyingine.
"Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2026, Skimu ya HIFADHI ilikuwa imeshaandikisha wanachama 592,791, na tunatarajia kuandikisha wanachama wapya zaidi ya 279,000 katika mwaka wa fedha 2026/27," alibainisha Mkurugenzi Mkuu.
TEHAMA na utunzaji wa mali
Kwa mujibu wa Mshomba, matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utendaji wa Mfuko yameongezeka hadi kufikia asilimia 99 kutoka asilimia 48 mwaka 2021, jambo lililowezesha waajiri na wanachama kujihudumia kwa urahisi pasipo kufika ofisini.
Katika eneo la utawala bora, Mfuko umeendelea kupata Hati Safi za Ukaguzi (Unqualified Audit Reports) kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ishara inayothibitisha usalama wa fedha za wanachama.
Mshomba alibainisha kuwa tathmini ya uendelevu wa Mfuko (funding level) nayo imeimarika kutoka asilimia 87.7 (Juni 2020) hadi asilimia 90.7 (Juni 2023).
Miradi mipya na mtazamo wa Dira 2050
Mkurugenzi Mkuu alieleza kuwa miradi kadhaa iliyokuwa imesimama - kama vile nyumba za makazi za Dungu, Toangoma, Mtoni Kijichi, na Jengo la Mzizima - irejelewa utekelezaji wake mwaka 2023 baada ya kaguzi maalum na inatarajiwa kukamilika kati ya Desemba 2026 na Machi 2027. Kuhusu mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, amesema tayari umeshazalisha tani 45,594 za sukari ya majumbani na kuingiza mapato ya shilingi bilioni 107.90 huku ukipata faida ya shilingi bilioni 4.56 mwaka 2025/26.
Mshomba alieleza kuwa kupitia Mpango Mkakati wa Nane (2026–2031) unaoenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na FYDP IV, NSSF inalenga kuongeza thamani ya Mfuko kufikia shilingi trilioni 24.75 na kuandikisha wanachama wapya milioni 5.8 kufikia Juni 2031.
Msajili wa Hazina
Akizungumza awali, mwakilishi wa Msajili wa hazina (TR) Sabato Kosuri aliwaambia wahariri hao kuwa mkutano huo ni sehemu ya mikakati ya Odfisi ya Msajili wa hazina kuzita fursa taasisi za umma kukuitana na wahariri ili kueleza shughuli za taasisi hizo kwa watanzania.
“Hii ni awamu ya pili ya mikutano hii na NSSF inakuwa taasisi ya kwanza kukutana na wahariri. Zipo taasisi zaidi ya 400 ambazo tutazifanyia mikutano kama hii ili kuwapa fursa watanzania kujua taasisi hizi za umma zinatendaje kazi zake,” alisema Kosuri.
- NSSF
- OTR
- TEF
- Mafao
- miradi
- michango