Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Makala

Pengo elimu afya ya uzazi tishio ustawi wa vijana - I

MKOA wa Dodoma una zaidi ya theluthi moja ya wakazi wake wakiwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 179, uk. 28

Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inaeleza kuwa wakazi wa mkoa huo wanafikia 765,179, huku vijana wakiwa asilimia 33.5.

Hata hivyo, kundi hilo ambalo linatarajiwa kuwa nguvu kazi ya taifa, ndilo linalokabiliwa na pengo kubwa la elimu ya afya ya uzazi, hali inayochochea mimba za utotoni, maambukizi ya magonjwa ya zinaa na kusitishwa kwa masomo kwa maelfu ya wasichana.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 29 ya wasichana mkoani Dodoma wamewahi kupata ujauzito. Hii inaamanisha kuwa msichama mmoja katika kila wasichana watatu mkoani humu, amepata ujauzito.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa tatizo siyo la mtu mmoja mmoja, bali ni changamoto ya afya ya umma.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wana uelewa mdogo kuhusu afya ya uzazi, huku asilimia 22.3 pekee wakitumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Watafiti walihitimisha kuwa ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi ni moja ya sababu kuu zinazochochea ujauzito wa utotoni katika mkoa huo.

Sheria zipo, uwajibikaji haupo Tanzania ina Sheria ya Afya ya Umma ya mwaka 2009, Sheria ya Kudhibiti VVU na UKIMWI ya mwaka 2008 pamoja na Sheria ya Ubora Huduma za Afya kwa Vijana - mwaka 2020 ambapo zote zinataka vijana wapate huduma rafiki na elimu sahihi ya afya ya uzazi.

Lakini uchambuzi wa utafiti mbalimbali unaonyesha pengo kubwa la utekelezaji. Ni asilimia 65 pekee ya vituo vya afya nchini vinavyokuwa na nakala za sheria hizo huku asilimia 31 ya vituo vya usimamizi wa huduma za afya ya uzazi vikishindwa kufanya majukumu yake kwa kufuata taratibu za kutoa elimu na huduma kwa mwaka. Hiki ni kiwango cha juu sana ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa asilimia 27.7, jambo ambalo linaibua mahitaji ya hatua za kuchukuliwa ili kulishughulikia tatizo hilo.

Watu ambao wamehojiwa na gazeti hili kuhusiana na suala hili wanasema halitokani na umasikini au uhusiano wa utotoni pekee, bali pia linatokana na pengo kubwa la elimu sahihi ya afya ya uzazi linalowaacha maelfu ya vijana wakifanya uamuzi muhimu wa maisha bila taarifa za kutosha.

  • Afya ya uzazi
  • Vijana
  • Dodoma

Soma Pia