Bustani ya Sheria
Sakata la Wakili Fatma Karume – III
KATIKA sehemu ya pili tuliona jinsi Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania alivyofungua shauri mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili akiiomba imvue kabisa uwakili Fatma Karume.
Serikali iliwasilisha ushahidi wa maneno aliyotumia mahakamani pamoja na machapisho yake ya Twitter, huku Fatma akisisitiza kuwa alikuwa akitoa maoni ya kitaaluma na kutetea maslahi ya mteja wake.
Sasa ilikuwa zamu ya kamati kutoa uamuzi.
Uamuzi uliotolewa na kamati hiyo uliingia kwenye historia ya taaluma ya uwakili nchini Tanzania.
Je, Tweets zilikuwa za Fatma? Hili ndilo swali la kwanza lililokuwa mbele ya kamati na lilionekana kuwa rahisi kwa sura, lakini zito kwa athari zake.
Je, akaunti ya Twitter iliyowasilishwa ilikuwa ya Fatma Karume?
Je, Fatma alikanusha kuwa baadhi ya machapisho hayo yalitoka kwake. Hata hivyo, Kamati ilichambua ushahidi uliowasilishwa, ukiwemo nyaraka na vielelezo vya video, na ikaridhika kwamba akaunti hiyo ilikuwa yake na kwamba ndiye aliyeandika machapisho hayo.
Kwa hiyo, kamati ikaendelea kujadili maudhui ya maneno hayo.
Je, Fatma alikiuka Maadili ya Uwakili?
Kamati ilikubali kuwa wakili ana haki ya kumtetea mteja wake kwa nguvu zote zinazoruhusiwa na sheria.
Lakini ikasema haki hiyo haimpi wakili ruhusa ya kumshambulia binafsi wakili mwenzake au viongozi wa taasisi za umma kwa lugha inayodhalilisha.
Kwa maoni ya Kamati, kauli za kumuita mwanasheria mkuu kuwa “far too junior,” asiye na uwezo na aliyeshindwa kabisa kuishauri serikali hazikuwa hoja za kisheria bali zilivuka mipaka ya maadili ya taaluma.
Kamati ikaongeza kuwa hata kama Fatma alikuwa na maoni kwamba Adelardus Kilangi hakustahili kuwa mwanasheria mkuu, bado alipaswa kuyawasilisha kwa lugha ya kitaaluma inayoheshimu hadhi ya taaluma ya uwakili.
Kamati haikuishia kuangalia maneno yaliyotumika kwenye kesi ya Ado Shaibu pekee, iligundua kuwa wakati shauri la nidhamu likiendelea kusikilizwa kwa siri, Fatma aliendelea kuandika machapisho kwenye Twitter akizungumzia yaliyokuwa yakitokea ndani ya kikao hicho.
Katika baadhi ya machapisho hayo aliikosoa kamati, Mahakama na viongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa lugha kali.
Kamati iliona hatua hiyo ilikuwa pia ni ukiukaji wa maelekezo yake pamoja na mwenendo unaodhihirisha kutokuheshimu chombo kilichokuwa kinamsikiliza.
Kamati hata ilibainisha kwamba wakati wa usikilizwaji wa shauri, Fatma aliwahi kuingilia mara kwa mara mwenendo wa kikao na hata kuonyesha kutoridhishwa na namna kilivyokuwa kinaendeshwa.
Kwa mtazamo wa kamati, matukio hayo yaliimarisha hoja kwamba kulikuwa na utovu mkubwa wa nidhamu.
Hukumu ya Kamati
Baada ya kuchambua ushahidi wote, kamati ilifikia hitimisho moja kwamba Fatma Karume alikuwa ametenda kosa kubwa la utovu wa nidhamu wa kitaaluma.
Kwa msingi huo, Kamati ikaamuru jina la Fatma Karume liondolewe kabisa kwenye Daftari la Mawakili (Roll of Advocates) kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria ya Mawakili, 2019.
Kwa lugha nyepesi, Fatma Karume alivuliwa leseni ya uwakili, hivyo kukosa haki ya kuendelea kufanya kazi kama wakili nchini Tanzania.
Uamuzi huo ulitolewa Septemba 23 2020, lakini hapo ndipo vita halisi vilipoanza, kwani Fatma hakukubaliana na uamuzi huo, na badala ya kukata tamaa, alihamishia mapambano yake Mahakama Kuu.
Na huko ndipo alipoibua hoja ya kisheria ambayo iligeuza kabisa mwenendo wa kesi, hoja hiyo haikuhusu kama alitumia lugha nzuri au mbaya.
Ilihusu swali moja muhimu; Je, Kamati ya Maadili ya Mawakili ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri lilivyofikishwa mbele yake?
Mwandishi ni Mwanasheria na Mchambuzi wa Sheria kutoka KGM Attorneys). Anapatikana kwa namba: au Email: karimbinmussa@ gmail.com.
- Fatma Karume
- Sheria
- Uwakili