Bustani ya Sheria
Sakata la Wakili Fatma Karume – VI
KATIKA sehemu ya tano tuliona jinsi Mahakama Kuu ilivyokataa kumpa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ruhusa (leave) ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi uliokuwa umemtendea haki Fatma Karume.

Lakini serikali haikuona huo kuwa mwisho wa safari. Iliamua kufanya kile ambacho wanasheria hukiita “second bite at the cherry.” Yaani kuomba tena ruhusa, safari hii moja kwa moja mbele ya Mahakama ya Rufani.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Kamati ya Maadili ya Mawakili waliwasilisha maombi mbele ya Mahakama ya Rufani.
Lengo lao lilikuwa lilelile. Kupewa ruhusa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliotengua uamuzi wa Kamati ya Maadili.
Kwa mtazamo wao, Mahakama Kuu ilikuwa imekosea kisheria, na walitaka Mahakama ya Rufani ichunguze makosa hayo.
Lakini Kabla hata hoja hizo hazijaanza kusikilizwa, kulijitokeza tatizo jingine; Pingamizi la kiufundi
Upande wa Fatma Karume uliweka pingamizi. Hoja ilikuwa kwamba maombi hayo hayakuwa yamekamilika kisheria, kwa sababu waombaji hawakuwa wameambatanisha Order (Amri) ya Mahakama Kuu waliyoitaka kuipinga.
Katika sheria za mwenendo wa mashauri, hati hiyo siyo jambo la hiari. Ni sehemu muhimu ya nyaraka zinazotakiwa kuambatanishwa ili Mahakama ijue rasmi uamuzi unaolalamikiwa.
Swali likawa hili; Je, kosa hilo lingeua maombi yote?
Mahakama ya Rufani ilikubaliana kwamba kulikuwa na kasoro ya kutokuwepo kwa Order.
Hata hivyo, Mahakama ya Tanzania ikaona kasoro hiyo ilikuwa inaweza kurekebishwa, badala ya kuua maombi yote mara moja.
Kwa msingi huo, Mahakama haikutupilia mbali maombi ya serikali. Badala yake, iliwapa waombaji nafasi ya kuwasilisha Order hiyo ndani ya muda waliopangiwa.
Kwa maneno mengine Mahakama ya Rufani ilichagua kutanguliza haki ya kusikiliza shauri badala ya kulimaliza kwa sababu ya kasoro iliyokuwa inaweza kurekebishwa.
Kwanini uamuzi huu ni muhimu?
Uamuzi huu ulikumbusha kanuni moja muhimu katika sheria za mwenendo wa mashauri.
Siyo kila kasoro ya kiufundi lazima iue shauri.
Pale ambapo kasoro inaweza kurekebishwa bila kuathiri haki za upande mwingine, Mahakama inaweza kutumia busara yake kuruhusu marekebisho badala ya kufunga mlango wa haki.
Ndiyo maana Mahakama ya Rufani haikusema serikali imeshinda, wala haikusema Fatma ameshinda.
Iliamua tu kwamba maombi ya serikali yaendelee kwa kufuata utaratibu sahihi, lakini wakati serikali Ikiendelea Kupambana, Fatma Karume naye alikuwa amefungua shauri lake tofauti kabisa katika Mahakama ya Rufani.
Safari hii hakupinga uamuzi wa Kamati ya Maadili, alikuwa anapinga uamuzi wa kwanza kabisa wa Jaji Feleshi uliomsimamisha kwa muda kufanya kazi ya uwakili.
Je, Mahakama ya Rufani ilikubaliana naye? Au ilisema alikuwa ametumia njia isiyo sahihi ya kuupinga uamuzi huo?
Hapo ndipo tunafika kwenye sehemu ya mwisho ya simulizi hili.
Itaendelea...
Mwandishi ni Mwanasheria na Mchambuzi wa Sheria kutoka KGM Attorneys).
- Fatma Karume
- Sheria
- Mahakama ya Rufani