Bustani ya Sheria
Sakata la Wakili Fatma Karume – VII
SEHEMU ya sita tuliona jinsi serikali ilivyoendelea kupambana Mahakama ya Rufani kwa kuomba ruhusa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliotengua uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Mawakili.
Lakini wakati huohuo, Fatma Karume naye alikuwa ameanzisha vita vyake tofauti kabisa mbele ya Mahakama ya Rufani.
Safari hii hakulalamikia Kamati ya Maadili, alikuwa analalamikia uamuzi wa kwanza kabisa wa Jaji Eliezer Feleshi uliomsimamisha kwa muda kufanya kazi ya uwakili wakati akiwa anamwakilisha Ado Shaibu.
Fatma Alienda Mahakama ya Rufani kwa njia gani?
Kwani yeye hakukata rufaa, badala yake, alifungua maombi ya revision (mapitio), akiiomba Mahakama ya Rufani iingilie kati na kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu uliomsimamisha kwa muda kufanya kazi ya uwakili. Hoja yake ilikuwa kwamba uamuzi huo haukuwa sahihi kisheria na ulipaswa kufutwa, lakini kabla Mahakama ya Tanzania haijachunguza kama alikuwa sahihi au la iliibuka swali moja la msingi.
Je, revision ndiyo ilikuwa njia sahihi ya kufika Mahakama ya Rufani?
Mahakama ya Rufani nayo ilijibu baada ya kuchambua Sheria ya Mawakili, Mahakama ya Rufani ilisema hapana. Mahakama ikaeleza kwamba kifungu cha 22(2)(b) cha Sheria ya Mawakili tayari kilikuwa kimeweka utaratibu maalumu wa kupinga uamuzi wa Jaji aliyemsimamisha wakili kwa muda.
Kwa hiyo, kabla ya kwenda Mahakama ya Rufani, Fatma alipaswa kwanza kutumia utaratibu huo wa kisheria. Kwa maneno mengine alikuwa amekimbilia Mahakama ya Rufani kabla ya kutumia njia ambayo sheria ilikuwa imeitenga mahsusi kwa aina hiyo ya malalamiko.
Kwa sababu hiyo, Mahakama ya Rufani haikuingia kujadili kama Jaji Feleshi alikuwa sahihi au alikosea.
Badala yake, ilisema njia iliyotumika haikuwa sahihi Na hivyo maombi ya revision yakashindwa.
Je, hatima ya Fatma Karume ikawa nini? Na hili ndilo swali ambalo wengi huuliza, baada ya kupitia kesi zote saba. Ni kweli kwamba Mahakama Kuu ilitengua uamuzi wa Kamati ya Maadili uliokuwa umemfuta Fatma Karume kabisa kwenye Daftari la Mawakili.
Lakini, Mahakama haikumrudishia moja kwa moja leseni yake ya uwakili, kwa sababu Mahakama ilisema kilichoharibika ni utaratibu wa kufikisha shauri mbele ya Kamati, si lazima iwe kwamba madai yenyewe hayakuwa na msingi.
Ndiyo maana ikaagiza Msajili wa Mahakama Kuu ndiye afikishe suala hilo kwenye Kamati ya Maadili kwa kufuata utaratibu uliokuwa umeelekezwa tangu mwanzo. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo hadi sasa, uamuzi huo bado haujazaa hitimisho jipya linalomaliza kabisa suala hilo. Hivyo, hali iliyobaki kusimama ni ile ya uamuzi wa awali uliomsimamisha Fatma Karume kwa muda kufanya kazi ya uwakili, kwa kuwa uamuzi wa Kamati uliomfuta kabisa ulifutwa, lakini suala lenyewe halikufungwa kwa uamuzi mpya wa mwisho.
Mafunzo muhimu katika sakata hili.
Mfululizo wa mashauri haya saba yamekuwa miongoni mwa mashauri muhimu zaidi katika sheria za maadili ya uwakili nchini Tanzania.
Zimefundisha mambo kadhaa muhimu ambayo ni pamoja na utaratibu wa kisheria ni muhimu kama haki yenyewe. Hata kama madai yana uzito, yakiletwa kwa utaratibu usio sahihi yanaweza kubatilishwa.
Wakili ana uhuru wa kumtetea mteja wake kwa nguvu zote za sheria, lakini uhuru huo unaambatana na wajibu wa kuheshimu maadili ya taaluma na taasisi za haki. Mahakama haiangalii tu nani ana hoja nzuri, bali pia kama sheria na taratibu zimefuatwa.
Kuchagua nafuu sahihi ni jambo la msingi. Ukichagua njia isiyotambuliwa na sheria, unaweza kupoteza shauri bila Mahakama hata kuingia kwenye kiini cha malalamiko yako.
Hitimisho.
Sakata la Wakili Fatma Karume si simulizi ya mtu mmoja pekee, ni simulizi kuhusu mgongano kati ya uhuru wa wakili kutetea mteja wake kwa nguvu zote, mamlaka ya mahakama kusimamia maadili ya taaluma, na umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria.
Ndiyo maana hadi leo, kesi hizi zinaendelea kufundishwa katika Law School of Tanzania, vyuo vikuu na mijadala ya kitaaluma, kwa sababu zinagusa misingi mikuu ya Legal Ethics, Civil Procedure na Constitutional Litigation.
Mwandishi ni Mwanasheria na Mchambuzi wa Sheria kutoka KGM Attorneys).
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Fatma Karume
- Sheria
- Mahakama ya Rufani