Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Michezo

Simba atakula nyasi hadi lini?

WAHENGA walisema simba mwenda pole ndiye mla nyama, wakimaanisha kuwa mtu mpole siku zote ndiye mwenye mambo makubwa ama utuluvi, hivyo huleta ushindi mkubwa katika kila jambo.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 17:15Dakika 1 kusomaToleo 178, uk. 39

Je, maneno ya wahenga yanapenya kwenye ngoma za masikio ya mashabiki wa Klabu ya Simba? Kwani ukimya wa Simba kwa misimu mitano mtawalia bila kunyanyua taji la Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, unawatia shaka.

Wakati dirisha la usajili likifungwa, bado ndani ya Klabu ya Simba kunaonekana hakujakaa sawa katika baadhi ya maeneo kama kiungo wa ulinzi na eneo la ushambuliaji, jambo ambalo linaweka hofu kwa wahafidhina wa kandanda.

Licha ya kufanya usajili wa wachezaji watatu wa kigeni na wanne wazawa, bado roho za mashabiki “hazijawa kwatu” kutokana na kile ambacho wanakiona kwa watani wao; Yanga ambao wameanzia walipoishia msimu uliopita huku usajili wao ukitishia amani upande wa pili.

Ni kweli Simba wamekosa meno kabisa katika soko la usajili kutokana aina ya usajili ambao wamekuwa wakifanya hasa katika baadhi ya maeneo ndani ya klabu hiyo, huku nyota wengi wanaojiunga na timu hiyo wakiwa hawana viwango vinavyoridhisha mashabiki wao wengi.

Duru zinaeleza shida siyo pesa ndani ya klabu hiyo, bali ni namna mambo yanavyoendeshwa hasa katika meza ya utawala huku vita ya madaraka ikionekana kugawa klabu hiyo na kuisambaratisha dhana ya “Nguvu Moja” ambayo ndio kauli mbiu ya timu hiyo ya Msimbazi, Dar es Salaam.

Ni wazi kuna pande mbili hadi tatu ambazo kila moja inavutia kwake kutaka kuwa na nguvu ndani ya klabu. Hii ni ajabu kuona klabu yenye katiba lakini ikiendeshwa kwa kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni ulaghai na kusababisha sintofahamu nyingi ndani ya kilabu hiyo.

Wapenzi wachache wa Simba sasa wameamua Mnyama huyo kula nyasi huku wakiwa wameshikilia vipande vya nyama mifukoni mwao.

Kutokana na hilo, hatma ya mafanikio kwa timu hiyo bado haieleweki kwa kuwa wapo waliofanikiwa azma yao – ya kuwagawa wana-Simba na kila mmoja analia na kulalama kwa harafu ya finyango za nyama wanazotupiwa.

  • Simba
  • Usajili
  • Ligi Kuu

Soma Pia