Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Michezo

Tanzanite Queens mashujaa waliokosa heshima

TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania chini ya miaka 20 ‘Tanzanite Queens' imeaga mashindano ya Kombe la Dunia baada ya kupokea vipondo vizito kwenye fainali hizo zinazoendelea nchini Poland.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 06:00Dakika 1 kusomaToleo 182, uk. 37

Licha ya kutolewa hatua ya makundi kwa kupokea vipigo kutoka kwa miamba ya soka duniani kama Brazil ambapo Tanzanite ilichapika mabao 4-1, huku ikichabangwa na England mabao 5-1 na dhidi ya Canada walipokea kipigo cha mabao 6-0 na kutupwa nje ya mashindano kwa kupoteza michezo yote hatua ya makundi na kuruhusu mabao 15 na kufunga mawili.

Ilikuwa mara ya kwanza Tanzanite Queens kushiriki na mara ya pili kwa timu kutoka Tanzania kushiriki Fainali za Kombe la Dunia ambapo Serengeti Girls chini ya miaka 17 walifanya hivyo na kuishia hatua ya robo fainali.

Timu za taifa kwa upande wa wanawake imekuwa na uwakilishi bora zaidi licha ya kuwa kama taifa hatujaona umuhimu wa kuwekeza katika soka la wanawake, bali kusubiri matukio ili kujionesha.

Timu hizi zimekuwa chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambao wamekuwa chachu ya mafanikio makubwa wakikosa usaidizi wa haja kwa wadau wengine nao kuichukulia kama fursa ya ajira kwa vijana wa kike nchini.

Tusingeshangaa kuona watoa hamasa wanaibuka kama Tanzanite Queens wangeendelea na mashindano, jambo ambalo halina afya zaidi ya kuzalisha wachumia tumbo wa taifa na siyo watu wazalendo wanaosimama vitani hata kama askari wameuawa.

Wino wa dhahabu kwa TFF na watendaji wote ambao wamekuwa chachu ya kuuinua mchezo wa soka la wanawake bila kujali ugumu na changamoto zilizoko mbele yao kwa maslahi mapana ya taifa na kizazi kijacho.

Tanzanite tayari wamerea nchini na hakuna hata pongezi walizopokea kama vile walivyopambana kivyao na TFF ndivyo ambavyo wamerejea kivyao.

  • Tanzanite Queens
  • Netiboli
  • Michezo

Soma Pia