Habari Kuu
Tundu Lissu katikati ya uhai, kifo Ijumaa
NI wiki ngumu. Wiki ya msongo zaidi kwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa anasubiri hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili.

Hatma ya kuendelea kupumua; pamoja na Mungu kuishikilia, lakini sasa ameongezeka mwingine kushikilia pumzi yake; Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam inayoshikilia kesi yake.
Ni saa 105 au zaidi kufikia Ijumaa, siku ambayo mahakama hiyo itakaa kwa ajili ya kutoa hukumu itakayohitimisha safari ya miezi 19 ya vuta nikuvute za kisheria kortini.
Ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu tangu Lissu alipokamatwa akiwa mkoani Ruvuma Aprili 9, 2025 kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam na kufunguliwa kesi hiyo ya uhaini.
Hukumu hiyo ya kihistoria inatarajiwa kutolewa Ijumaa wiki hii, Novemba 6, 2026, ikiwa ni siku 38 tangu alipohitimisha kutoa hoja zake za mwisho zenye kurasa 1000, akijenga mawazo yake ya kisheria akiieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shitaka la uhaini linalomkabili.
Hukumu hiyo ndiyo yenye kuamua hatma mpya ya Lissu, ambapo iwapo atatiwa hatiani, atakabiliwa na adhabu ya kunyongwa hadi kufa, na iwapo mahakama itaona ushahidi wa Jamhuri haukujitosheza kumtia hatiani, ataachiwa huru.
Sheria ya Uhaini Namba 2 ya mwaka 1970, inataja adhabu ya kunyongwa hadi kufa kuwa pekee na hakuna afueni yake.
Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiwa na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Kesi hii imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na umma wa Watanzania, wanachama wa Chadema, wanasheria taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Utetezi wa mwisho Katika kuhitimisha hoja za mwisho za utetezi Septemba 29, 2026, Lissu aliiambia Mahakama Kuu kuwa ushahidi uliotolewa dhidi yake umeshindwa kuthibitisha vigezo vya kisheria vinavyounda kosa la uhaini.
Lissu aliwaambia majaji hao kuwa kauli zake zinazotumiwa na upande wa mashtaka kujenga kesi dhidi yake hazitoshelezi matakwa ya Kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu.
Alisema sheria imeainisha kwa uwazi matendo yanayoweza kuunda kosa la uhaini na kwamba, kwa hoja yake, maneno anayodaiwa kuyasema hayaingii katika matendo hayo.
Hata hivyo, katika hoja zake, Lissu alisema Jamhuri ilipaswa kuthibitisha si tu kwamba alitamka maneno yanayodaiwa, bali pia kwamba maneno na matendo yaliyowasilishwa mahakamani yanakidhi vigezo vya kosa mahsusi la uhaini aliloshtakiwa nalo, kama vilivyoainishwa katika sheria.
Ataja matendo yanayounda uhaini Katika kuijenga hoja yake, Lissu alianza na Ibara ya 28(4) ya Katiba, ambayo kwa mujibu wa mawasilisho yake inatambua uhaini kama kosa la juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Muungano, lakini ikiacha kosa lenyewe lifafanuliwe na sheria.
Kutokana na hilo, alielekeza hoja zake katika Kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu.
Lissu aliiambia mahakama kuwa kifungu hicho kinaainisha matendo mbalimbali yanayoweza kuunda uhaini, yakiwemo kumuua au kujaribu kumuua rais, kuendesha vita dhidi ya Jamhuri ya Muungano, kukusudia kusababisha kifo, majeraha au kufungwa kwa Rais, na kukusudia kumuondoa Rais madarakani kwa njia zisizo halali.
Aliyataja makosa mengine kuwa ni kukusudia kuipindua serikali, kukusudia kuitishia serikali, bunge au mahakama, kushirikiana na maadui wa Jamhuri, kuchochea uvamizi wa kutumia silaha, kutumia nguvu kubadili Serikali na kutoa msaada kwa maadui wa nchi.
Kwa msingi huo, Lissu alitaka Mahakama ipime kauli zinazodaiwa kutamkwa naye dhidi ya vigezo hivyo vya kisheria badala ya kutegemea tafsiri au hisia kuhusu uzito wa maneno hayo.
‘Kuzuia uchaguzi’ iko wapi?
Lissu alihoji ni sehemu gani ya Kifungu cha 39 inayotaja maneno hayo kuwa miongoni mwa matendo yanayounda kosa la uhaini.
“Tuanze na neno tutavuruga uchaguzi, liko wapi kwenye hiyo list ya matendo 10 ya kihaini?
Kuzuia uchaguzi, iko wapi? Kuhamasisha uasi… iko wapi kwenye Section 39?” alihoji katika mawasilisho yake.
Hoja yake ni kwamba hata kama maneno hayo yalikuwapo katika hotuba yake, Jamhuri bado ilikuwa na wajibu wa kuonesha namna yanavyokidhi kosa mahususi lililowekwa na sheria.
Akifafanua alisema: “Kama haya matendo niliyoshitakiwa nayo hayafiti katika sehemu yoyote katika mojawapo ya matendo 10 ambayo kifungu cha 39 kimeyataja kwamba ukiyafanya haya unakuwa umefanya kosa la uhaini… maana yake ni kwamba mimi sijafanya kosa lolote la uhaini.”
Hiyo ni hoja ya utetezi ambayo sasa Mahakama italazimika kuipima dhidi ya tafsiri ya upande wa mashtaka na ushahidi wote uliowasilishwa katika kesi.
Watatu kati yao walikuwa maofisa wa polisi ambao, kwa mujibu wa hoja yake, hawakuhudhuria mkutano wa Aprili 3, 2025.
Alisema shahidi mwingine alikuwa mwandishi wa habari aliyekuwapo katika mkutano huo.
Lissu anadai maofisa hao walihitimisha kuwa nia ya kuitishia Serikali ilikuwapo kwa sababu uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazosimamiwa na Serikali.
Lakini utetezi wake unasema hakuna katika maneno yanayomweka hatiani ambako Serikali, chombo cha Serikali au ofisa wa Serikali alitajwa moja kwa moja.
Kutokana na hilo, Lissu aliwaambia majaji hao kuwa kesi ya Jamhuri imejengwa juu ya tafsiri ya mashahidi badala ya ushahidi unaothibitisha nia inayotakiwa na sheria.
Eneo jingine ambalo Lissu amelishambulia ni namna upande wa mashtaka ulivyoeleza kitendo kinachodaiwa kudhihirisha nia hiyo.
Kwa mujibu wa shitaka, nia hiyo ilidhihirishwa kupitia kitendo cha kutamka maneno yanayolalamikiwa.
Lakini Lissu amepinga hoja hiyo akisema maneno yaliyotamkwa hayawezi yenyewe kuchukuliwa kuwa deed au kitendo kinachokidhi hitaji la overt act chini ya kifungu anachoshtakiwa nacho.
Kwa hiyo, katika utetezi wake Lissu anaitaka Mahakama iamue kama kutamka maneno hayo kulitosha kisheria kuthibitisha kitendo kinachodhihirisha nia ya uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d).
Alitaja makosa yanayohusu uandikishaji wa wapiga kura, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa, kujifanya mtu mwingine, kuingilia mikutano halali na makosa ya siku ya uchaguzi.
Mahakama ndiyo mwamuzi wa mwisho Hoja hizi ni sehemu ya mawasilisho ya mwisho ya Lissu baada ya ushahidi wa pande zote kufungwa.
Msingi wa utetezi wa Lissu ni kwamba Jamhuri haikuthibitisha mnyororo unaohitajika kisheria; nia inayotajwa katika Kifungu cha 39(2) (d), mlengwa wa tishio hilo, kitendo kinachodhihirisha nia hiyo na uhusiano kati ya maneno aliyotamka na kosa la uhaini.
Upande wa mashtaka, kwa upande mwingine, umeshtaki kwa msingi kwamba kauli hizo zililenga kuhamasisha umma kuzuia uchaguzi na hivyo kuitishia Serikali.
Katika hatua za awali za kesi, Mahakama pia ilikataa pingamizi la Lissu dhidi ya uhalali wa hati ya mashtaka, ikisema suala la nia lilikuwa la kuthibitishwa kwa ushahidi wakati wa usikilizaji.
Hivyo, hoja iliyobaki mbele ya Mahakama si tu kama Lissu alitamka maneno yanayodaiwa, bali kama ushahidi uliotolewa unayapa maneno hayo vigezo vyote vinavyohitajika kisheria kuyafanya kuwa kosa la uhaini.
Hitimisho la upande wa mashtaka Akiwasilisha hoja za mwisho za upande wa mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga alisema anaomba kumshukuru (mshtakiwa Lissu), licha ya kwamba yeye huwa hakubali hilo.
“Kwa kipindi chote ambacho tulikuwa naye katika kesi hii, mbali na maneno makali aliyotumia, hayakuweza kujenga neno baya zaidi ya kutengeneza tafsiri ya sheria. Sisi Jamhuri tulikuwa na lengo moja tu la kuthibitisha shtaka kupitia kifungu hiki ambacho ni kipya na kwa mara ya kwanza kinatumika katika kesi hii,” alisema.
Katuga alisema Jamhuri ilikuwa na lengo moja katika kesi hiyo, ambalo ni kuthibitisha shtaka kwa kutumia kifungu hicho cha sheria.
Alieleza pia kuwa kunyongwa si adhabu pekee inayoweza kutolewa endapo atapatikana na hatia katika kesi ya uhaini inayomkabili.