Biashara
Uchimbaji madini North Mara kuendelea kwa miaka 15
Uchumi wa Tanzania, pamoja na kutegemea vyanzo vingine vya mapato, makusanyo kutoka kampuni za madini ni nguzo muhimu ya kuinua uchumi. Soma kuelewa namna serikali ilivyoamua kuongeza mkataba na kampuni ya kuchimba madini.

SERIKALI ya Tanzania imehuisha leseni maalumu za uchimbaji za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa miaka mingine 15, hatua inayowezesha kuendelea kwa shughuli zake na uwekezaji wa muda mrefu.
Mgodi huo, uliopo wilayani Tarime, Mara, unaendeshwa kupitia ushirikiano kati ya serikali na kampuni ya Barrick, inayojulikana sasa kama Barrick Mining Corporation.
Katika taarifa yake ya Oktoba 6, 2026, Barrick ilisema kuhuishwa kwa leseni hizo kutaimarisha uwekezaji katika mgodi, wafanyakazi na jamii zinazouzunguka. Hatua hiyo inaweka msingi wa kuendelea kuchimba na kuchakata madini kwa ajili ya biashara ya dhahabu.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua masharti ya mauzo wala utaratibu wa kupanga bei ya dhahabu inayozalishwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Biashara Barrick - nje ya Amerika Kaskazini, Seb Bock, alisema hatua hiyo ni muhimu kwa North Mara na ushirikiano wa kampuni hiyo na Tanzania.
Alieleza kuwa tangu mwaka 2019, kampuni imekuwa ikishirikiana na serikali na wananchi kuimarisha uhusiano na kupanua fursa za kiuchumi.
Serikali na Barrick zilianzisha Twiga Minerals mwaka 2019 kusimamia migodi ya North Mara na Bulyanhulu. Serikali ina hisa za asilimia 16 katika kila mgodi, huku manufaa ya kiuchumi yakigawanywa sawa kati ya washirika hao.
Kwa mujibu wa Barrick, shughuli zake nchini zimechangia takribani dola bilioni 5.3 katika uchumi tangu mwaka 2019, kupitia kodi, mrabaha, mishahara, gawio na ununuzi wa bidhaa na huduma.
Kampuni pia ilisema zaidi ya asilimia 90 ya ununuzi wake hutoka kwa kampuni zilizosajiliwa Tanzania.
Aidha, imeeleza kuwa Barrick imekuwa ikisaidia jamii zinazozunguka migodi, na kwamba kamati za maendeleo hushiriki kuchagua miradi ya kipaumbele, ikiwemo shule, vituo vya afya na barabara, kulingana na mahitaji ya wananchi husika na kufadhiliwa na kampuni hiyo ya madini.
- north mara
- dhahabu
- madini
- mkataba