Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

UN yashangaa ukimya wa serikali kwa waliosababisha mauaji Okt 29

Mwaka mmoja sasa umefika baada ya kutokea kwa vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania; Oktoba 29, 2026, zilizoambatana na matukio ya watu kuuawa, kupotea na wengine kuwa na ulemavu wa kudumu. Maswali bado mengi kama Umoja wa Mataifa (UN) unavyohoji.

Jumatatu, 2 Novemba 2026 · 15:04Dakika 4 kusomaToleo 188, uk. 12
Hali ilivyokuwa baadhi ya sehemu za Jiji la Dar es Salaam siku ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Hali ilivyokuwa baadhi ya sehemu za Jiji la Dar es Salaam siku ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

TIMU ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) imeshangazwa na ukimya wa Serikali ya Tanzania kuhusu kukamatwa, kuchukuliwa hatua na hata kutangazwa kwa waliosababisha mauaji ya watu wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania, Oktoba, mwaka jana - 2025.

Wataalamu hao wakiwa wanasheria, wanazuoni wa haki na uhuru wa binadamu, wamesema “Tanzania ina kigugumizi” cha kuweka hadharani waliohusika na mauaji hayo, ikiwa ni pamoja na watu kuteswa, kupotezwa na wengine kupewa ulemavu wa kudumu.

Taarifa yao kwa umma wa dunia ilisambazwa Alhamisi iliyopita – Oktoba 29, ambayo ilikuwa tarehe ya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kutokea kwa machafuko na vurugu za uchaguzi mkuu wa Tanzania zilizosababisha mauaji, kuumizwa, kupotezwa na kuharibiwa kwa miundombinu muhimu katika miji mikubwaya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya.

Wakati wataalamu hao wanaweka taarifa yao hadharani, tayari Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipokea ripoti ya Tume ya Jaji Chande iliyoundwa na serikali kubaini madhila ya vurugu hizo.

Katika taarifa yake, Jaji Chade alisema kuwa vurugu hizo zilisababisha vifo vya watu 518 (raia 502 na askari 16), huku zaidi ya watu 2,000 wakijeruhiwa. Pia watu 758 waliripotiwa kutekwa au kupotea, ambapo 113 walipatikana na 445 bado hawajapatikana hadi sasa. Aidha, ilielezwa kwamba chanzo cha vurugu hizo ilikuwa ni pamoja na masuala ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.

Wataalam hao wameishinikiza Serikali ya Tanzania kuweka hadharani ripoti kamili ya Jaji Chande, ambayo ilipewa jina la Tume ya Uchunguzi wa Vurugu na Ghasia zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Wamesema kutoiweka hadharani ripoti hiyo yote, ni kukiuka haki ya waathirika kujua ukweli na kuchochea hali ya kutowajibishwa kwa waliohusika ambapo wameonyesha wasiwasi wao kwamba licha ya kupita mwaka mmoja tangu kutokea matukio hayo, hakuna kiongozi au mtumishi wa serikali aliyefunguliwa mashtaka kuhusiana na ukiukwaji huo.

Wakati taarifa hiyo ya UN ikisema hivyo, Rais Samia wakati akipokea ripoti ya Tume ya Jaji Chande, Aprili 23, mwaka huu 2026, alisema ripoti hiyo ni yake na wasitokee watu kudai kuwa na umiliki nayo.

“Ndugu wananchi na ndugu viongozi, mmeshuhudia nakabidhiwa mavitabu yote yale, hii ni ripoti ya rais, aliyeunda tume ni rais, na ripoti yote hii ni ya rais, kwa hiyo wasitokee watu wengine wakadai kuwa na umiliki (owneship), hii ni ripoti ya rais…” alisema Rais Samia.

Akaongeza; “Tumepokea, nataka niwahakikishie Tume kwamba tumepokea mapendekezo yote, na tutakayoyasoma kwenye makabrasha haya, tutaanza kuyafanyia kazi mara moja,”alisisitiza.

Aidha, taarifa ya watalaam wa UN imeendelea kusisitiza uchunguzi huru, wa haraka, wa kina na usioegemea upande wowote ili kuhakikisha waathirika wanapata haki ya kujua ukweli, haki na fidia.

“Hakuna haki wala uwajibikaji kwa waliosababisha watu kupotezwa kwa lazima, mauaji yaliyofanywa, kukamatwa kiholela na watu kuteswa na vitendo visivyo vya kibinadamu na vinavyodhalilisha utu...”

“Vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zilitawaliwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi na nguvu za kuua, kukatika kwa huduma za intaneti pamoja na vitendo vya vitisho na unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania,” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Tume ya Jaji Lila Baada ya Jaji Chade kukabidhi ripoti yake, serikali inaunda Tume ya Jaji Shaaban Lila inayochunguza jinai wakati wa vurugu hizo, ambapo taarifa ya watalaam wa UN inasema; “hakuna taarifa za kina kuhusu mamlaka, majukumu na upeo wa kazi ya tume hiyo mpya.

Wataalam hao wa UN wameitaka tume hiyo na mamlaka za Tanzania kuweka wazi madhumuni na maeneo inayoyachunguza, pamoja na kuhakikisha matokeo ya uchunguzi wake yanawekwa hadharani mara kazi hiyo itakapokamilika.

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo pia imeonyesha wasiwasi kuhusu taarifa za kuendelea kuwepo kwa watu wanaoshikiliwa na vyombo vya serikali au kuwa mahakamani kwa muda mrefu kwa kukabiliwa na madai ya makosa yanayohusiana na ugaidi.

“Waathirika wanaendelea kukabiliwa na hali mbaya na inayozidi kudhoofika ya haki za binadamu, huku kukiwa na ongezeko la vikwazo katika shughuli za kiraia,” wamesema.

Aidha, wamedai ukandamizaji dhidi ya wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wafuasi wa vyama vya upinzani unaendelea kuathiri uhuru wao wa kufanya kazi na kushiriki katika shughuli za kijamii na kisiasa.

Wameongeza kuwa baadhi ya watu waliokimbilia nchi jirani wanaendelea kukabiliwa na vitendo vya ukandamizaji vinavyovuka mipaka ya nchi.

Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amekuwa akikanusha kuwepo kwa hila ya kuwaonea ama kukiuka haki za wale wanaoikosoa serikali.

  • Vurugu Okt.29
  • Uchaguzi
  • Vifo
  • Haki
  • Siasa

Soma Pia