Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Michezo

Utamu NBC PL warejea na FVS

UTAMU wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara umerejea wikiendi iliyopita kwa msimu wa NBC PL 2026/27 kuanza, kwa klabu 16 kumenyana katika michezo 30 dakika 2700.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 17:15Dakika 1 kusomaToleo 178, uk. 40
Utamu NBC PL warejea na FVS
Utamu NBC PL warejea na FVS — Picha kutoka Maktaba

Wakati mashabiki wakianza kufurahia ama kununa kwenye matokeo ya mechi, jambo kubwa lenye kuvutia msimu huu wa kandanda, ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutambulisha teknolojia ya usaidizi wa mwamuzi ya ‘Football Video Support’ (FVS) ambayo ni mfumo mpya unaotumika sasa badala ya VAR.

FVS ina faida nyingi za kumsaidia mwamuzi kuwa na usahihi wa uamuzi na matukio yanayoweza kubadili mwelekeo wa mchezo ndani ya dakika 90 husika, ambayo inampa mwamuzi haki, uhakika na heshima bila kuharibu mtiririko wa mchezo.

Hizi ni faida tano kwa mwamuzi kutumia FVS; ni kupunguza makosa makubwa kama uhalali wa bao, pigo la mkwaju wa penati, kadi nyekundu ya moja kwa moja na kumtambua mchezaji. Pili husaidia kudhibiti kasi ya mchezo, FVS haiangalii kila kitu, bali mwamuzi ndiye anaomba tukio analohitaji kujiridhisha.

Pia, humsaidia mwamuzi kupunguza presha na kukosolewa kwani FVS ni ushahidi wa pili wa kuthibitisha uamuzi wake, hii hupunguza shinikizo la lawama na shutuma kwa waamuzi.

Faida nyingine ni kumsaidia mwamuzi kujifunza kutoka mchezo mmoja hadi mwingine kwa kuangalia upande ambao aliukosa katika tukio husika ili kuboresha uono wake katika matukio yatakayofanana na hilo kwa mechi zinazofuata.

Aidha, FVS hupatikana kwa gharama ndogo jambo ambalo kwa sasa hata ligi ndogo zinaweza kumpa mwamuzi msaada, hivyo teknolojia ya FVS ni msaada wa uamuzi kwa waamuzi wote kote ulimwenguni.

Hata hivyo, FVS hutumia kamera nne hadi sita na mtaalamu mmoja, wakati VAR huhitaji chumba cha VAR, kamera nane hadi 12 pamoja na zingine za mstari wa kuotea huku ikihitaji watu watatu hadi wanne.

Je, ni kwa kiasi gani FVS inaenda kupunguza lawama ambazo zimekuwa zikitupwa kwa waamuzi kwa kushindwa kutoa tafsiri sahihi za sheria za soka na faida kwa timu isiyostahili, ni jambo la kusubiri kuona vile kutaenda kwa msimu mzima.

  • NBC PL
  • FVS
  • Waamuzi
  • TFF

Soma Pia