Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Tahariri

Watanzania wanataka ushindi wa soka bila aibu

TANZANIA inajiandaa kuwa mwenyeji mwenza wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2027, pamoja na Kenya na Uganda.

Jumatatu, 28 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 184, uk. 2

Hii ni nafasi adhimu kwa nchi na timu yetu kuonyesha uwezo wa kuandaa mashindano, lakini kubwa zaidi kujenga timu itakayocheza kwa ushindani mbele ya mashabiki wake.

Ndiyo maana hivi sasa, tunasikitishwa na nguvu inayotumika kwenye mvutano kuhusu jezi za Taifa Stars.

Baadhi ya viongozi wenye dhamana ya michezo wameingia katika malumbano ya hadharani kuhusu ubora, taratibu na mkataba wa kandarasi kadhaa, wakati nguvu kubwa ingepaswa kusaidia namna ya kuipa nguvu timu yetu.

Tunakubali kwamba jezi ni utambulisho wa taifa na endapo ikiwa kuna kasoro, TFF, serikali na wazabuni wakae mezani, wapime sampuli, waangalie masharti ya mkataba na watangaze hatua za kurekebisha.

Kwa miezi iliyobaki, tungependa kusikia mjadala mkubwa zaidi kuhusu maandalizi ya timu. Taifa Stars inahitaji ratiba yenye maana ya mechi za majaribio, programu imara ya utimamu wa mwili, akili, uchambuzi wa wapinzani na maandalizi ya kisaikolojia.

Wachezaji wanaocheza nje na ndani ya nchi waunganishwe mapema katika mfumo mmoja, badala ya kukutana mwisho wa safari na kutarajiwa kufanya miujiza.

TFF na mabenchi ya ufundi waweke wazi vigezo vya uchaguzi wa wachezaji, nafasi ya vijana wanaochipukia na namna benchi la ufundi litakavyopimwa.

Timu ya taifa haiandaliwi kwa hotuba za hamasa pekee, inahitaji makocha wenye muda wa kutosha, wataalamu wa tiba na lishe, vifaa vya mazoezi, pamoja na michezo inayowajaribu wachezaji dhidi ya wapinzani wa viwango tofauti.

Tunawaomba pia viongozi wasichanganye nafasi zao. Serikali inaweza kusimamia maslahi ya umma na kuuliza maswali kuhusu fedha na maandalizi, huku shirikisho la soka likipaswa kutekeleza majukumu yake ya kiufundi na kimkataba.

Endapo kuna wakandarasi waliopewa jambo la kutekeleza, wapewe fursa ya kukaa pamoja na serikali na kujibu hoja na kurekebisha kilichokosewa bila kuhukumiwa kwanza kwenye majukwaa.

Sisi Pambazuko tunaamini kwamba malengo yetu makubwa ni kuhakikisha Taifa Stars inayoweza kupambana kufika mbali na, ikiwezekana, kulitwaa kombe hapa nyumbani.

Uhakika ni kwamba hatuwezi kubakiza kombe ambalo hatujalishinda na haitakuwa kazi rahisi ikiwa muda mwingi sasa unatumika kusaka mambo ambayo siyo msingi mkubwa wa malengo yetu.

Watanzania wanapenda kuona maandalizi makubwa na yenye mikakati mikubwa na ubunifu kwa timu ili kushinda na hapo wataunga mkono timu yao kwa kila hali.

Mashabiki wa Taifa Stars watashangilia zaidi iwapo maandalizi yataonekana katika pasi, kasi, ulinzi na mabao.

Watanzania sasa, ikiwa imebaki miezi michache kufikia Afcon, wanahitaji kujua kila kinachoendelea kwenye maandalizi hayo na siyo malumbano.

Wanataka kujua ratiba ya mechi za majaribio na taarifa za mara kwa mara kuhusu hatua zilizofikiwa ili kuwa na timu bora.

Sasa basi, TFF na wizara wasisubiri siku ya mechi kueleza kwa nini programu iliyopangwa haikutekelezwa. Uwajibikaji unaanza sasa, wakati bado kuna nafasi ya kubadili mwelekeo na kurekebisha udhaifu.

Viongozi wetu wapunguze minyukano, waongeze maandalizi, Afcon ya 2027 haitahukumiwa kwa picha ya uzinduzi wa jezi. Itahukumiwa kwa kiwango cha Taifa Stars uwanjani na uwezo wa nchi kuwakaribisha wageni.

Tukiwekeza akili zetu hapo, hakika furaha kuu itakuwa ushindi na hata kubakiza kombe Tanzania, hayo mengine huenda – kwa Watanzania ni ziada tu.

  • Taifa Stars
  • Afcon
  • TFF
  • Soka

Soma Pia