Utekelezaji wa Dira 2050 wahitaji maamuzi magumu
Katika utekelezaji wa Dira 2050 sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 huku sekta ya umma ikipaswa kuchangia asilimia 30.
Serikali imezitaka bodi na menejimenti za taasisi na mashirika ya umma kufanya maamuzi magumu na ya haraka katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050), lakini ikisisitiza kuwa kasi hiyo lazima iende sambamba na sheria, uwajibikaji na utawala bora.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka, alisema miaka ya mwanzo ya utekelezaji wa Dira 2050 ni muhimu kwa sababu maamuzi, uwekezaji na taasisi zinazojengwa sasa vitaathiri kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania katika miaka ijayo.
Akifunga Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026) jijini Arusha, alisema Dira 2050 imeingia katika hatua ya utekelezaji, hivyo viongozi wanapaswa kuchukua hatua zinazoendana na ukubwa wa malengo yaliyowekwa.
“Dira 2050 si jambo la siku zijazo tena. Utekelezaji wake umeanza,” alisema.
Alisema kufanikisha malengo hayo kunahitaji viongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi yenye uzito kwa wakati na kuonya dhidi ya kupitisha maazimio yasiyolingana na mabadiliko yanayohitajika.
“Tusije na maazimio mepesi mepesi,” alisema.
Hata hivyo, Balozi Kusiluka alisema kufanya maamuzi kwa haraka hakumaanishi kupuuza taratibu, bali taasisi zinapaswa kutumia mifumo ya Serikali kupata ufafanuzi wa masuala ya kisheria ili kufanya maamuzi kwa wakati na kwa usahihi.
“Tunataka taasisi zetu ziwe na ujasiri wa kufanya maamuzi na kusonga mbele, lakini zifanye hivyo ndani ya misingi imara ya sheria, uwajibikaji na utawala bora,” alisema.
Pimeni matokeo, si shughuli
Balozi Kusiluka aliagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha taasisi za umma zinapimwa kwa viashiria vinavyoonyesha matokeo halisi badala ya kujilinganisha na taasisi nyingine ambazo pia hazifanyi vizuri.
“Benchmark yetu isiwe taasisi nyingine ambazo hazifanyi vizuri. Tulinganishe na wenzetu mahali kwingine duniani wanaofanya vizuri zaidi,” alisema.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema mabadiliko hayo yanahitaji mashirika kuhama kutoka kupima mafanikio kwa idadi ya shughuli zilizotekelezwa na badala yake kuangalia matokeo na thamani iliyozalishwa kwa Taifa.
Alisema hilo linahitaji kuongeza tija, ufanisi, ubunifu na matumizi ya teknolojia, huku rasilimali za Serikali zikisimamiwa kwa uangalifu na uwekezaji ukizalisha thamani inayopimika.
Kwa mashirika ya kibiashara, alisema mafanikio yanapaswa kupimwa kwa tija, uendelevu na faida, huku taasisi za huduma za umma zikipimwa kwa ubora, upatikanaji na ufanisi wa huduma.
Vijana kupewa nafasi
Balozi Kusiluka pia alisema Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi iko tayari kutoa vibali vya kuajiri vijana katika nafasi za uongozi, hususan kwenye vitengo vya ubunifu, hata kama hawana uzoefu wa muda mrefu, iwapo wana ujuzi adimu unaoweza kuongeza tija.
Pia alitaka sekta ya umma na binafsi kuongeza ushirikiano na kuhakikisha mipango yao inaendana na Dira 2050.
Kuhusu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alisema taasisi hazipaswi kuzichukulia kama mambo ya kujibu kwa ajili ya kukamilisha ukaguzi pekee.
Badala yake, alisema mapendekezo ya CAG yatumike kuimarisha mifumo, kudhibiti vihatarishi na kuzuia hoja zinazojirudia.
Balozi Kusiluka alisema mashirika ya umma yana nafasi muhimu katika utekelezaji wa Dira 2050 kutokana na shughuli zake katika uzalishaji, biashara, usafirishaji, nishati, uwekezaji na utoaji huduma.
Maazimio yawe matokeo
Aliwataka viongozi kuhakikisha maazimio ya C-CEOs Forum yanaingizwa katika mipango ya utekelezaji ya taasisi zao badala ya kubaki kwenye makabrasha.
“Msiyachukulie maazimio haya kama hitimisho la Kikao Kazi; yachukulieni kama mwanzo wa kazi,” alisema.
Alisema kipimo halisi cha mafanikio ya mkutano huo kitaonekana baada ya washiriki kuondoka Arusha kupitia ubora wa maamuzi, kasi ya utekelezaji, utatuzi wa changamoto, ushirikiano na thamani inayozalishwa kutokana na rasilimali za umma.
“Msiache mawazo mazuri yabaki katika ukumbi huu... msiruhusu maazimio mliyokubaliana yawe kumbukumbu nzuri ya Kikao Kazi; yafanyeni yawe sehemu ya matokeo ya taasisi zenu,” alisema.
Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa mageuzi yanayoendelea, lakini akasema bado kuna kazi kubwa kutokana na matarajio ya wananchi.
C-CEOs Forum 2026 ilifanyika Arusha kuanzia Septemba 28 hadi 30, ikiwakutanisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi na mashirika ya umma 320 pamoja na wadau wengine.