Uchunguzi wa Nishati na Mazingira
Je, mkakati wa 2034 utafika vijijini wakati mkaa ukiwa 'rahisi' kuliko gesi?
Licha ya Tanzania kuweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034, kaya nyingi za Kiroka, Morogoro, bado zinategemea mkaa na kuni.

SERIKALI ya Tanzania imeweka lengo la kihistoria la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya wananchi watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia.
Lengo hilo limebainishwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), ambao unakusudia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda misitu, kuboresha afya za wananchi na kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, hali halisi katika maeneo mengi ya vijijini inaonyesha kuwa safari ya kufikia malengo hayo bado ni ndefu. Katika Kata ya Kiroka, Wilaya ya Morogoro Vijijini, wananchi wengi bado wanaendelea kutegemea mkaa na kuni kama vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia. Sababu si kwamba hawafahamu faida za gesi ya kupikia (LPG) au teknolojia nyingine za nishati safi, bali ni changamoto za kiuchumi zinazowafanya washindwe kufanya mabadiliko hayo.
Uchunguzi uliofanyika katika kata hiyo unaonyesha kuwa bei ya mkaa imeendelea kuwa ya chini ikilinganishwa na gharama za kununua na kujaza mitungi ya gesi. Wakati huo huo, uvunaji haramu wa miti unaendelea kuchochea upatikanaji wa mkaa kwa gharama ndogo, hali inayoufanya uonekane kuwa chaguo nafuu kwa kaya nyingi licha ya madhara yake makubwa kwa mazingira.
Kwa mtazamo wa wananchi wengi wa Kiroka, uchaguzi wa aina ya nishati hautegemei zaidi masuala ya mazingira, bali uwezo wa kifedha wa familia. Wakati mapato ni madogo na mahitaji ya msingi yanaongezeka, familia nyingi hulazimika kuchagua njia inayowawezesha kupika chakula kwa gharama ndogo zaidi.
Mtego wa umaskini na matumizi ya nishati
Utafiti uliochapishwa mwaka 2021 na jarida la kisayansi la MDPI, unaojulikana kama Forests, Farms, and Fallows, unaonyesha kuwa umaskini wa kiuchumi katika maeneo ya vijijini ni miongoni mwa sababu kuu zinazochochea uharibifu wa misitu. Watu wengi hukata miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa kama njia ya kujipatia kipato, huku wanunuzi wakiendelea kuutumia kwa sababu ni nafuu kuliko nishati nyingine.
Hali hiyo inaonekana wazi Kiroka. Wananchi wengi wanaeleza kuwa mapato yao yanategemea kilimo, biashara ndogo ndogo na shughuli nyingine zisizo na uhakika wa kipato. Katika mazingira hayo, kununua mtungi wa gesi, jiko la gesi pamoja na kugharamia ujazaji wa mara kwa mara huwa mzigo mkubwa kwa kaya nyingi.
Zawadi Mohamed, Mjasiriamali mmoja wa kike katika kata hiyo anasema kuwa anatambua vizuri faida za kutumia gesi ya kupikia.
Kwa mujibu wa Zawadi, gesi hupunguza moshi jikoni, huokoa muda wa kupika na hata kupunguza gharama za muda mrefu. Hata hivyo, changamoto kubwa ni uwezo wa kuendelea kujaza mtungi kila unapokwisha.
"Ukishajaza mtungi unaona ni rahisi kutumia, lakini ukiishiwa ghafla wakati huna fedha, unalazimika kurudi kwenye mkaa. Hapo ndipo changamoto ilipo," anasema.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa tatizo si ukosefu wa uelewa kuhusu faida za nishati safi, bali uwezo mdogo wa kifedha wa kaya nyingi.
Kwa mtazamo wa kwanza, mkaa unaweza kuonekana kuwa ndiyo nishati ya bei ya chini zaidi. Lakini wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa bei hiyo ni ya "bandia" kwa sababu haiakisi gharama halisi za uharibifu wa misitu, upotevu wa vyanzo vya maji, mmomonyoko wa ardhi na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya moshi wa mkaa na kuni.
Pia, uwepo wa uvunaji haramu wa miti hupunguza gharama za uzalishaji wa mkaa. Wakati wazalishaji hawalipi gharama halisi za kulinda mazingira wala kodi zote zinazostahili, bidhaa hiyo huingia sokoni kwa bei ndogo kuliko inavyopaswa kuwa.
Matokeo yake ni ushindani usio sawa kati ya mkaa na nishati safi kama gesi ya kupikia. Gesi hulazimika kupitia mfumo rasmi wa kodi, usafirishaji na usambazaji, wakati sehemu ya biashara ya mkaa huendeshwa nje ya utaratibu rasmi.
Mkakati wa taifa unakabiliwa na mtihani
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia umebeba matumaini makubwa kwa Watanzania. Unalenga kuongeza matumizi ya gesi, majiko banifu, biogas, umeme na nishati nyingine safi ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Lakini utekelezaji wake unahitaji zaidi ya kutangaza sera. Wananchi wa vijijini wanahitaji kuona mabadiliko halisi katika uwezo wao wa kumudu gharama za teknolojia hizo.
Bila hatua madhubuti za kupunguza gharama za kuingia kwenye matumizi ya gesi, wananchi wengi wataendelea kubaki kwenye matumizi ya mkaa kwa sababu ndiyo unaoonekana kuwa nafuu kwa wakati huo.
Mbali na changamoto za kiuchumi, suala la uwajibikaji linaonekana kuwa muhimu katika kufanikisha mabadiliko ya matumizi ya nishati.
Kwa muji utafiti ukuwa ukosefu wa uwazi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miradi ya nishati, unaweza kuchelewesha mafanikio yaliyokusudiwa. Wananchi wanahitaji kuona namna fedha za umma zinavyotumika na jinsi ruzuku zinavyowafikia walengwa.
Pale ambapo hakuna taarifa za wazi kuhusu matumizi ya fedha au utekelezaji wa miradi, huibuka mashaka yanayopunguza imani ya wananchi katika programu za serikali.
Kwa sababu hiyo, wataalamu wanaamini kuwa uwajibikaji na utoaji wa taarifa kwa umma ni sehemu muhimu ya mafanikio ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
Moja ya mapendekezo yanayotolewa mara kwa mara ni utoaji wa ruzuku kwa vifaa vya nishati safi. Ruzuku inaweza kusaidia kupunguza gharama za kununua mitungi ya gesi, majiko ya kisasa na vifaa vingine vinavyohitajika ili kaya nyingi ziweze kuanza kutumia nishati safi.
Aidha, baadhi ya wadau wanaona kuwa ruzuku inaweza kuelekezwa pia katika kupunguza gharama za kujaza mitungi ya gesi, hasa kwa kaya zenye kipato cha chini.
Hatua hiyo inaweza kufanya wananchi wengi waone kuwa kutumia gesi si jambo la watu wenye kipato kikubwa pekee, bali ni huduma inayoweza kufikiwa na kila mtu.
Mhandisi Estomih Sawe, Mkurugenzi wa TaTEDO-SESO amesisitiza kuwa mafanikio ya mpango wa taifa yatategemea uwezo wa sera za kifedha kuwasaidia wananchi wa kawaida kumudu gharama za teknolojia za nishati safi.
Kwa mujibu wa Sawe, bila kuwepo mazingira yanayorahisisha upatikanaji wa teknolojia hizo, wananchi wataendelea kutumia nishati walizozoea kwa sababu ndizo wanazoweza kuzimudu.
“Kwa mtazamo huo, sera za nishati zinapaswa kwenda sambamba na sera za kupunguza umaskini na kuongeza kipato cha wananchi,” anasema.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Musa Kilalaka amesema mkoa wa Morgoro una vyanzo vingi vya maji vinavyopaswa kulindwa, hivyo ajenda ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia itasaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti, kulinda afya za wananchi pamoja na kutunza vyanzo hivyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Amesema ni vema jamii ikafikiwa na elimu ya matumizi nishati safi ya kupikia na hivyo kuchangia kufikia kwa malengo ya taifa ya kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
"Suala la nishati Morogoro Vijijini linahitaji teknolojia mbadala. Tunashirikiana na jamii kuhamasisha majiko banifu, lakini sera za fedha lazima ziunge mkono uwezo wa mwananchi wa kawaida kununua nishati hizi”,amesema
Utafiti uliochapishwa na MDPI (2021), "Forests, Farms, and Fallows," unaonesha uharibifu wa kasi wa misitu unatokana na umaskini wa kiuchumi vijijini ambao unamfanya mwananchi ashindwe kumudu nishati mbadala.
Kata ya Kiroka inaonyesha picha halisi ya changamoto zinazokabili utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. Wananchi wengi wanafahamu umuhimu wa kutumia gesi na teknolojia nyingine safi, lakini uwezo mdogo wa kifedha, bei ya chini ya mkaa, hofu kuhusu usalama wa gesi na upatikanaji mdogo wa huduma hizo bado vinazuia mabadiliko.
Mjasiriamali wa Kike Getrude Cosmas anasema matumizi ya nishati safi husaidia kurahisisha shughuli za kupika kwa kupika haraka na kuokoa muda huku ikipunguza magonjwa kama vile ya vifua, ingawa mtungi ukiisha kuujaza ni gharama kubwa ambayo bad oni itendawili kwetu "Gesi inatusaidia kuokoa muda na kupunguza magonjwa, lakini mtungi ukisha hatuna hela ya kujaza mara moja".amesema Getrude
Ikiwa Tanzania inataka kufikia lengo la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034, juhudi zinapaswa kuelekezwa si tu katika kuhamasisha matumizi ya gesi, bali pia katika kuboresha uwezo wa wananchi kuimudu. Serikali inapaswa kuimarisha mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa miti ili kuondoa ushindani usio wa haki unaoufanya mkaa uonekane kuwa nafuu kuliko ulivyo.
Joyce Sabinus Mfanyabiashara mdogo wa mkaa anasema analazimika kuuza mkaa wa makopo kwa kopo moja shilingi 1000 ili aweze kujikimu kimaisha kutokana na kutokuwa na shughuli yingine ya kufanya huku akiwa na watoto wawili wanaohitaji huduma za chakula na vifaa vya elimu kutoka kwake. "Kama bei ya mkaa ikipanda sana na gesi ikashuka, hapo tutabadilika" anasema.
Jitihada za kusogeza nishati safi kwa jamii
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati Tanzania, Benki ya dunia imejitolea kutoa kati ya dolza kimarekani Bilioni 30-40 ili kufadhili mirad ya umeme na nishati safi barani Afrika.
Lengo likiwa ni kuwapatia umeme na nishati safi ya kupikia watu zaidi ya Milioni 300 ifikapo mwaka 2030 na hivyo kuchochea maendeleo endelevu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Kupitia benki ya maendeleo (AfDB) nchi kama Tanzania, Rwanda na Somalia ni miongoni mwa zinazoongoza kwa kasi ya mabadiliko haya
Kwa mujibu wa shirika la maendeleo la Nishati ya Jadi na mazingira Tanzania (TaTEDO) kupitia TaTEDO -SESO kwa kushirikiana na Norway inaendeleza kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini ambao Julai 15 2026 ilipokearuzuku ya shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya kuongeza kasi ya matumizi ya nishati endelevu na suuhisho la upishi safi nchini.
Vilevile, uwazi katika matumizi ya bajeti za nishati, utoaji wa taarifa kwa umma na usimamizi wa ruzuku ni mambo muhimu yatakayojenga imani ya wananchi na kuhakikisha msaada unawafikia walengwa.
Bila kuziba mianya ya uwajibikaji, kuongeza elimu kuhusu matumizi salama ya gesi na kuweka mazingira yanayofanya nishati safi iwe nafuu kwa wananchi wa kawaida, mkaa utaendelea kuwa mfalme wa majiko ya Kiroka, huku misitu ikiendelea kutoweka na ndoto ya kufikia malengo ya mwaka 2034 ikibaki kuwa changamoto kubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Serikali lazima iweke hadharani ripoti za wazi kuhusu matumizi ya bajeti ya miradi ya nishati mbadala na kuhakikisha ruzuku zinafika kwa walengwa wa Kiroka. "Mkaa ni gharama, Gesi ni akiba," lakini akiba hiyo itafikiwa tu ikiwa mianya ya uwajibikaji itazibwa.
Umebakiwa na makala 1 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Nishati Safi
- Mkaa
- Gesi
- Kiroka
- Morogoro
- Misitu
- Umaskini
- Nishati Tanzania
- Mazingira
- Tabianchi
- TaTEDO
- Nishati Mbadala