Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Wazo Binafsi

Ya Rwanda yapaswa kuigwa Tanzania kunusuru vijana

KILICHOFANYWA na Serikali ya Rwanda wiki iliyopita kupiga marufuku baadhi ya pombe kali kusambazwa na kuuzwa nchini humo, kinawahusu zaidi vijana Tanzania.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 14:15Dakika 2 kusomaToleo 177, uk. 32

Ongezeko la matumizi makubwa ya vileo vikali miongoni mwa vijana nchini limekuwa tishio kubwa kwa afya ya umma, maendeleo ya taifa na maadili ya jamii.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaeleza kuwa zaidi ya asilimia 35 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24, wamewahi kutumia pombe kali angalau mara moja.

Vinywaji vyenye kiwango kikubwa cha kilevi vimekuwa vikitumiwa kwa wingi na vijana katika miji mikubwa na vijijini.

Sababu za msingi zinazochangia ongezeko hilo ni pamoja na shinikizo la rika, katika jamii ya sasa, vijana wengi huona matumizi ya vileo kama ishara ya ukomavu na hivyo kushindwa kujizuia kwa hofu ya kubaguliwa.

Hali hutokea sana pale ambapo kijana akimuona mwenzake – wa rika moja, akitumia kilevi naye kujiuliza; “kama huyu anafanya hivi na huyu ni sawa na mimi, kwa nini mimi nibaki nyuma?”

Iwapo swali hili halitakuwa na tafakuri nzuri nyuma yake, bila kujua au kutarajia, kijana anaweza kujikuta ametumbukia kwenye unywaji wa pombe wenye madhara.

Aidha, changamoto za kiuchumi kama ukosefu wa ajira na umaskini pamoja na shinikizo la masomo zimesababisha baadhi ya vijana kutumia pombe kama njia ya kukwepa uhalisia.

Pia upatikanaji rahisi wa vileo hivyo, tena kwa bei ndogo, umerahisisha hata wanafunzi kuthubutu kuvitumia!

Mitandao ya kijamii ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikihusisha matumizi ya vileo na mafanikio na starehe, vijana wengi huvutiwa na kuamua kuonja vileo.

Wataalamu wa afya wamekuwa wakieleza madhara ya matumizi ya vinywaji vikali kuwa ni kuharibu viungo muhimu vya mwili ikiwamo ini na figo na kuongeza hatari ya kupata magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, vidonda vya tumbo na saratani.

Kielimu, wanafunzi wengi wamekuwa wakipata matokeo duni na hata kusimamishwa masomoni kutokana na tabia ya ulevi.

Kijamii, vileo vikali vimekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya familia, vurugu, ajali za barabarani na uhalifu.

Ripoti za vyombo vya dola zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya matukio ya kihalifu yanayofanyika usiku, yanahusiana moja kwa moja na ulevi.

Kisaikolojia, matumizi ya muda mrefu ya vinywaji vikali husababisha uraibu ambapo mtu anaishia kunywa si kwa raha bali ili kuepuka dalili za kujiondoa. Hali hii huambatana na mfadhaiko na mawazo ya kujidhuru au hata kujiua.

Ili kukabiliana na changamoto mbalimbali kunahitaji jitihada za pamoja; serikali inapaswa kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni zinazodhibiti uuzaji holela wa vileo.

Taasisi za elimu na kidini nazo zina wajibu wa kutoa elimu ya kina kwa vijana kuhusu madhara ya vileo hivyo pia ni muhimu kuwepo kwa programu za kuwajengea vijana stadi za kujiajiri na kuwapa fursa za michezo na sanaa ili wawe na namna mbadala ya kutumia muda wao.

  • Vijana
  • Pombe
  • Afya

Soma Pia